Dk Gwajima asimulia uteuzi ulivyomshtua

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema ilimchukua siku tatu bila usingizi wa uhakika, baada ya kupokea taarifa ya kuteuliwa kuwa mbunge na Waziri wa Afya, Desemba mwaka 2020.

Kiwango hicho cha mstuko, kilitokana na ukweli kuwa hakuwahi kutarajia kwamba siku moja angekuwa mwanasiasa. Hivyo hakufikiria kuteuliwa katika nafasi ya ubunge na hatimaye uwaziri.

Dk Gwajima ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, amesema mtihani mwingine aliupata pale alipoteuliwa tena na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021, katika wizara iliyokuwa mpya na hakujua pa kuanzia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akifurahia jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia wakati alipotembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Tabata jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Dk Gwajima ameeleza hayo leo, Ijumaa, Aprili 17, 2026 kwenye mahojiano maalumu, yaliyofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Mwananchi Communications Limited, jijini Dar es Salaam.

Anasimulia siku ya taarifa ya uteuzi wake kuwa mbunge na waziri kwa mara ya kwanza, kuwa zilianza tetesi mitandaoni kwamba wakati wowote Baraza la Mawaziri lingetangazwa, naye hakuwa miongoni mwa wanaotajwa na hata yeye hakujitarajia.

Dk Gwajima, amesema siku ilianza akiwa ofisini akiwa naibu katibu mkuu. katibu mkuu wake alimweleza anaenda kikazi Iringa, akimuacha ofisini kusimamia majukumu, akiahidi kurudi haraka endapo kungekuwa na jambo la dharura.

“Nilikuwa najiuliza, kama kweli baraza linatangazwa, nani atampokea waziri wakati kiongozi wangu hayupo? Nikamuuliza katibu mkuu, sasa wewe unaenda huko baraza likitangazwa itakuwaje, akaniambia anaenda Iringa si mbali, kukiwa na chochote atarudi haraka,” amesema.

Baadaye, alirejea nyumbani na kukawa na taarifa mitandaoni kuhusu matangazo mubashara. Kwa kuwa tetesi zilikuwa uteuzi wa Baraza la Mawaziri, naye aliwasha televisheni kufuatilia matangazo hayo yalipoanza.

Amesema alikuwa anafuatilia, akiwa na matarajio ya kusikia majina ya viongozi wa sekta alizokuwa anazifanyia kazi, yaani Afya na Tamisemi.

“Nimekaa hapo jina la kwanza, la pili, la tatu, la nne la tano, nasikia mheshimiwa Rais amewateua wengine wawili (kuwa wabunge) na kuwapandisha kuwa mawaziri. Nikasema nani hao jamani tuwapongeze.

“Jina la kwanza la kwangu, nilisikia joto na baridi vikipishana kwa wakati mmoja. Sijawahi kutarajia, sijagombea, sijawahi kuwa mwanasiasa, haya mambo yamekuwaje halafu Uviko-19 ndio imepamba moto,” amesema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akizugumza na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Tabata jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Amesema taarifa hiyo ilisababisha ajiulize namna atakavyoifanya kazi ya uwaziri, kwani kwa wakati huo aliona haelewi.

“Sikutaka kusikiliza aliyefuata, nilienda kulala huku naanza kuona simu za pongezi, maana nilifikiri maigizo nikajua kwamba ni kweli, nililia na kutabasamu kwa pamoja, kwa sababu niliona kazi kubwa, niliona heshima niliyopewa.

“Kwa siku tatu nilikaa kama nimezubaa. Ukifika usiku ukilala ukiamka tu palepale, ndio habari ya kulala imeisha, yaani unashangaa hiyo heshima na ule utukufu unaokuwa umepewa kwenda kuwatumikia Watanzania,” amesema.

Hali inayofanana na hiyo, amesema alikutana nayo alipoteuliwa na Rais Samia kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, akisema alijiuliza maswali mengi kwa kuwa wizara hiyo ilikuwa mpya kwake.

Ameeleza uteuzi ulimkuta na maswali mengi, hasa kutokana na taaluma yake ya udaktari, akijiuliza angeanzia wapi na angefikaje katika wizara inayohusika na masuala ya kijamii.

“Nilijiuliza, mimi kama daktari naingiaje kwenye wizara ya maendeleo ya jamii? Lakini nikapata imani kwamba nitaongozwa na kupewa miongozo sahihi ya kutekeleza majukumu yangu,” amesema.

Dk Gwajima amesema alitumia msingi wa taaluma yake ya afya ya jamii kuelewa majukumu hayo, akibainisha kuwa dhana ya afya haipaswi kuishia hospitalini bali inaanzia katika kuzuia magonjwa.

“Katika taaluma ya afya ya jamii, tunafundishwa kwamba lengo si mtu kuugua kisha kutibiwa, bali kuzuia asipate ugonjwa kabisa. Hapo ndipo dhana ya kubadili fikra inapokuja,” amesema.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akizugumza wakati wa mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Tabata jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Uelewa huo, amesema ulimsaidia kuona nafasi ya wizara hiyo katika kuzuia matatizo ya kijamii yanayosababisha wananchi kuishia kuwa wagonjwa au kuwa katika mazingira magumu.

Alisema baada ya kulielewa hilo, alianza kufanya kazi kwa karibu na maofisa maendeleo ya jamii ili kubaini ni sera na mikakati ipi inahitajika kuwasaidia wananchi kabla hawajafikia hatua ya kuhitaji huduma za matibabu.

“Hapo ndipo nikatambua kuwa udaktari wa kwanza uko kwenye kuzuia. Ukishindwa kuzuia, ndipo hatua ya matibabu inafuata,” amesema.

Katika mahojiano hayo, Dk Gwajima amesema kihistoria yeye alikuwa mtumishi wa umma wa kawaida, akitekeleza majukumu yake bila kuwaza kugombea nafasi yoyote ya kisiasa.

“Watu wanapozungumzia kugombea, wanadhani kila mtu alikuwa amejiandaa kuingia kwenye siasa. Mimi sikuwahi kuwa na mpango huo. Nilikuwa mtumishi wa umma nikifanya kazi zangu kama kawaida,” amesema.

Mara yake ya kwanza ya kuingia kwenye uongozi wa kisiasa, amesema ilikuja baada ya kuteuliwa na hayati Magufuli.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima akizugumza na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd leo Ijumaa Aprili 17, 2026 Tabata jijini Dar es Salaam. Picha na Said Powa

Hata hivyo, amesema baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya uongozi wake, hakukimbilia kugombea nafasi za kisiasa, akisisitiza bado alikuwa mtumishi wa umma hadi atakapostaafu mwaka 2031.

“Niliona ni busara kusubiri uamuzi wa mamlaka. Unaweza kukimbilia kugombea ukakosa, na hata huku usipate. Nilichagua kubaki tayari kutumikia popote nitakapohitajika,” amesema.

Lakini, amesema bado anaona kuna nafasi ya kushiriki siasa za uchaguzi siku zijazo, endapo mazingira na muda vitaruhusu.

“Bado tunaishi, bado kuna uchaguzi. Wakati ukifika, kama itampendeza Mungu tutaamua. Kwa sasa tunaendelea kuhudumu,” amesema.

Kuhusu mitandao ya kijamii

Dk Gwajima  kwenye mtindo wake wa uongozi hakosekani kwenye mkitandao ya kijamii mara nyingine akijibizana na vijana, alipoulizwa kuhusu hilo, amesema kufanya hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya uwaziri wa maendeleo ya jamii, yanayomtaka kuwa karibu na wananchi.

“Hayo majukumu ya uwaziri ni pamoja na kuelimisha jamii. Jukumu la kwanza ni kuwa karibu na wananchi unaowatumikia. Mimi ni waziri wa maendeleo ya jamii, mimi sio waziri wa elimu kwamba unikute darasani naongea na watoto,” amesema.

Hata hivyo, amesema anafurahia kutumia mitandao hiyo na kwamba anashangazwa na wale wa chini yake wanaomshangaa badala ya kuiga anachokifanya.

Amesisitiza anafanya hivyo kwa sababu mitandao ya kijamii ndilo jukwaa linalomwezesha kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi.

Ingawa kwenye mitandao hiyo wakati mwingine anakutana na maoni kinzani dhidi yake, amesema ni jambo la kawaida kwa sababu ndivyo watu walivyo.

“Watu wachokozi wanakuja wanakutibua ila mimi ukinitibua na wewe nikifanikiwa nakutibua vilevile ila ni muda mchache tu, dakika tano nishakusahau tunasonga mbele na mambo mengine,” amesema.

Nani anaendesha kurasa zake za mitandao? Akijibu hilo amesema yeye mwenyewe ndiye anayeziendesha, kwa maana kuchapisha picha na hata kujibu maoni ya wafuasi wake.

“Yaani simu yangu mimi anisaidie nani, mimi mwenyewe ndio admin (kiongozi) wa kurasa zangu zote. Naendesha mwenyewe sitaki hata maneno na mtu kwa sababu simu hii umeshaambiwa ni ya mkononi,” amesema.

Amesema yeye si mtu wa kupenda kufanyiwa kila kitu, ndiyo maana yanayohusu simu na kurasa zake za mitandao ya kijamii anayafanya mwenyewe na hakuwahi kuona taabu kufanya hivyo.

Dk Gwajima amesema uongozi wa kisasa haupaswi kuwa wa kukaa ofisini, bali ni dhamana inayopaswa kutekelezwa muda wote.

“Unapopokea taarifa ya mtu mwenye shida, huwezi kupuuza. Una macho, unasikia, unaelewa na una dhamana ya uongozi huwezi kulala bila kuhakikisha umemsaidia,” amesema.

Amesema dhana ya uongozi ni kujitoa kikamilifu kwa ajili ya wengine, akisisitiza viongozi wanapaswa kuwa tayari kuwahudumia wananchi muda wote kama sehemu ya wajibu wao.

“Uongozi ni utumishi. Ni lazima uwe tayari kufanya kazi muda wote, kama ambavyo Mungu anavyotutazama na kutujalia kila wakati. Sisi tumewekwa hapa kumwakilisha kupitia Serikali,” amesema.

Katika kuyatimiza hayo, amesema ni muhimu viongozi na watumishi wa umma kubadilika na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, akibainisha kuwa kizazi cha sasa kipo kwenye ulimwengu huo.

Changamoto kubwa, amesema ipo kwa baadhi ya watumishi waliopo ngazi za chini ambao bado hawajabadilika kifikra, hali inayochelewesha utoaji wa huduma.

“Lazima tuwajenge wasaidizi wetu waingie kwenye ulimwengu wa sasa. Wapo ambao hata hawana akaunti za kufuatilia masuala ya kazi zao mtandaoni. Hii haiendani na wakati tulionao,” amesema.

Kwa mujibu wake, baadhi ya watumishi wanaogopa kujitokeza mitandaoni kwa hofu ya kukosolewa, akisema hilo halipaswi kuwa kikwazo.

“Watu wanaogopa kushambuliwa, lakini hayo hayana maana. Kilicho muhimu ni uwezo wako wa kufikiri na kusaidia jamii, si maoni ya watu kuhusu mwonekano wako,” amesema.

Amewasihi viongozi wenzake, kuzingatia hoja za wananchi badala ya kujibu mashambulizi ya mitandaoni, akisema majibu ya jazba hayasaidii.

“Badala ya kugombana na mkosoaji, angalia hoja yake ni nini. Kama kiongozi, kazi yako ni kuitatua. Mwisho wa siku ataona thamani yako kupitia msaada uliompa,” amesema.