Geita. Wachimbaji dhahabu mkoani Geita wameshauriwa kuwa na matumizi sahihi ya fedha kwa kufanya uwekezaji kwenye amana za muda na hati fungani za Serikali (Treasury Bond) zinazosimamiwa na Benki Kuu, nyumba na ardhi, kwa ajili ya manufaa yao ya sasa na badaye kutokana na fedha wanazopata kupitia uchimbaji.
Rai hiyo imetolewa April 16, 2026 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Herman Matemu alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela aliyekuwa mgeni rasmi katika Semina ya uwekezaji kwa wachimbaji madini mkoani humo, iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Matemu amewakumbusha wachimbaji kuzingatia kanuni na tahadhari za uwekezaji ikiwa ni pamoja na kutokuweka fedha zao katika eneo moja la uwekezaji, kufanya tafiti za kina kabla ya kufanya uwekezaji pamoja na kuepuka utapeli kwenye uwekezaji kwwa kufanya ufuatiliaji katika kila hatua ya uwekezaji.
Katika hatua nyingine, Matemu amesema mkoa huo umeendelea kudhibiti utoroshaji wa madini katika kulinda uchumi wa nchi ambapo amewataka wachimbaji kudumisha tabia ya kizalendo kwa kuepuka utoroshaji wa madini.
“Mzalendo wa kwanza ni yule anayefuata sheria, kanuni na taratibu na hasa katika sekta ya madini, tunahitaji uaminifu mkubwa ili hayo madini, sisi kama taifa, tuone tofauti ya Geita ambayo ina madini na halmashauri zingine ambazo hazina madini,” amesema Matemu.
Ofisa kutoka BoT, Amoni Mwambonda,aliyemwakilisha Mkurugenzi wa BoT tawi la Mwanza katika Semina ya wachimbaji madini mkoa wa Geita,akizungumza namna walivyobaini baadhi ya wachimbaji kukosa utamaduni wa kutunza akiba.
Ofisa kutoka BoT Tawi la Mwanza, Amoni Mwambonda, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi, amesema kupitia semina hiyo wamebaini baadhi ya wachimbaji kutokuwa na utamaduni wa kutunza kumbukumbu za matumizi ya kila siku ambapo amewasihi kuanza kutunza kumbukumbu ili kudhibiti uchumi binafsi.
“Usipotunza kumbukumbu ya matumizi utakumbana na changamoto nyingi za kimaisha na unaweza kushindwa kufanikiwa vizuri, ni vizuri kuweka bajeti ya aidha ya wiki, au mwezi hiyo itawasaidia kufuata utaratibu uliojiwekea,” amesema.
Naye, mwenyekiti wa wachimba madini mkoani humo, Titus Kabuo, ameiomba Benki Kuu na Serikali kuendelea kuwalinda na kuwawezesha wanunuzi na wauzaji wa dhahabu nchini kwa kuwapatia mikopo nafuu kwa kuwa wao ndiyo sababu ya wachimbaji wadogo kufanikiwa katika shughuli zao.
“Hatupati mikopo sisi wachimbaji, mkopo tunaupata kutoka kwa dealers na brokers kwenye shughuli zetu za uchimbaji hatimaye mnapata hizo dhahabu zinazowafikia, kwa hiyo msiwaue hawa, muwawezeshe vizuri kama ni mikopo muwaongezee,” amesema Kabuo.
Baadhi ya washiriki ambao ni wachimbaji madini, wanunuzi na wauzaji madini mkoani Geita,waliohudhuria semina iliyoandaliwa na Benki kuu Tanzania, BoT,ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha na uwekezaji.
Mwenyekiti wa chama cha Wanawake Wachimbaji Geita (Gewoma), Asia Masimba ametumia semina hiyo kuiomba Serikali kuwawezesha wachimbaji wadogo kupitia utoaji wa mikopo pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambayo imekuwa kikwazo kwa baadhi ya migodi ya Rwamgasa na Matabe, hivyo kuathiri shughuli za uchimbaji madini.
