Iran yafungua Mlango wa Hormuz, yasema…

Tehran. Serikali ya Iran imetangaza kufungua rasmi njia ya kimkakati ya bahari ya Mlango wa Hormuz kwa shughuli za usafirishaji wa kibiashara, hatua inayokuja wakati wa kipindi cha usitishaji mapigano kati yake na Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amebainisha hilo leo Ijumaa, Aprili 17, 2026, kupitia mtandao wa X, akisema kuwa njia hiyo sasa iko wazi kwa meli zote za kibiashara kwa muda uliobaki wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

“Kwa kuzingatia usitishaji mapigano nchini Lebanon, njia ya kupita kwa meli zote za kibiashara kupitia Mlango wa Hormuz imetangazwa kuwa wazi kabisa kwa kipindi kilichosalia cha usitishaji mapigano,” amesema Araghchi.

Ameongeza kuwa meli zitaruhusiwa kupita katika njia maalumu iliyopangwa tayari kwa uratibu wa Shirika la Bandari na Masuala ya Bahari la Iran.

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Marekani yanatarajiwa kumalizika Aprili 22, 2026.

Mlango wa Hormuz ulianza kufungwa kwa vitendo mwishoni mwa Februari 2026 kufuatia mashambulizi ya pamoja ya kijeshi yaliyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran.

Katika kujibu mashambulizi hayo, Iran ilichukua hatua za kuimarisha uwepo wa kijeshi katika eneo hilo, ikiwemo kuweka vizuizi vya usafiri wa baharini na kuongeza ukaguzi mkali kwa meli zinazopita, hali iliyosababisha kusimama au kucheleweshwa kwa safari nyingi za meli za mafuta na mizigo.

Kufungwa kwa njia hiyo kwa wiki kadhaa kumesababisha athari kubwa kimataifa, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta duniani kutokana na hofu ya upungufu wa usambazaji.

Baadhi ya nchi zinazoagiza mafuta kwa wingi zililazimika kutafuta njia mbadala au kutumia akiba zao za dharura ili kukabiliana na hali hiyo.

Kufunguliwa kwa Mlango wa Hormuz kunatoa ahueni ya muda kwa biashara ya kimataifa kutokana na umuhimu wa njia hiyo.

Endapo usitishaji mapigano utaendelea au kuongezwa muda, kuna uwezekano wa kurejea kwa utulivu katika soko la mafuta na usafirishaji wa baharini.