Songwe. Benki ya Dunia (WB) imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kuboresha elimu kupitia Mpango wa BOOST (Basic Education for Growth and Transformation) baada ya kufanya ukaguzi wa miradi hiyo katika halmashajri za Mbozi na Tunduma mkoani Songwe, inayolenga kuinua ubora wa elimu ya msingi nchini.
Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya elimu inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mpango wa BOOST, yenye lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika shule za msingi.
Timu ya wataalamu kutoka WB pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, imeridhishwa na kiwango cha utekelezaji wa miradi ya BOOST katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, ikiitaja halmashauri hiyo kuwa mfano bora wa kuigwa na maeneo mengine nchini.
Wadau hao wa maendeleo akiwepo Gemma Todd pamoja na Dmitry Chugunov, wakiwa wilayani Mbozi, wametembelea shule tatu za msingi ambapo wameeleza kuridhishwa namna miradi hiyo inavyotekelezwa kwa ufanisi na kuupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa usimamizi.
“Baada ya kukagua miradi ambayo imekidhi vigezo tunamuomba Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Mbozi kuhamasisha wakuu wa shule nyingine kufika na kujifunza kutoka katika shule zilizofanya vizuri ili kuongeza tija ya mpango huu,” amesema Chugunov.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Mbozi, Dorothy Mwandila amezitaja shule zilizotembelewa katika ziara hiyo kuwa ni shule za msingi Haloli, Lutumbi, Ihanda pamoja na Dk Samia S.H, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya, endelevu na yenye manufaa kwa jamii.
Mwandila amesema shule ya msingi Haloli imepokea fedha jumla ya Sh50 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vinne vya madarasa, ofisi moja pamoja na ujenzi wa matundu 19 ya vyoo ambapo mtundu manane ya wavulana na matundu 11 ya wasichana.
Moja ya mradi Boost wa shule uliotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kutembelewa na wajumbe wa benki ya Dunia na Tamisemi
“Ujenzi wa shule mpya awali na msingi Ihanda ilipokea Sh329.5 milioni kwa ajili ya ujenzi jengo la utawala, madarasa mawili ya awali, madarasa sita ya shule ya msingi, vyoo vya wanaume 6 na wasichana sita, pamoja na vyoo matundu manne ya awali,” amesema Mwandila.
Amesema shule nyingine iliyotembelewa ni shule ya msingi Lutumbi ilipokea Sh 226.21 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa matatu, ukarabati vyumba vinane na ukamilishaji vya vyumba vinne vya madarasa kupaua.
Kwa upande wake mtaalamu wa elimu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi, Ally Swalehe amepongeza juhudi zinazofanywa na halmashauri hiyo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya shule zinazonufaika na zile za jirani, hususan za elimu ya awali ili kuongeza wigo wa manufaa ya miradi hiyo.
Aidha, walimu kutoka shule zinazonufaika na miradi hiyo wameeleza kuwa utekelezaji wa BOOST umeleta mabadiliko chanya katika ufundishaji, ikiwemo kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo kupitia madarasa yanayozungumza, pamoja na kuimarika kwa hali ya usafi na mazingira ya shule kwa ujumla.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mpemba, Frances Mwandosya amesema programu ya BOOST imeleta mabadiliko makubwa, ikiwemo kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarika kwa ufaulu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mariam Chaurembo amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027 wamejipanga kukarabati zaidi ya madarasa 40 ya elimu ya awali na msingi ili kuhakikisha watoto wanajifunza katika mazingira rafiki.