Arusha. Mahakama ya Rufani imethibitisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa Paulo Laizer baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Ndomononi Siyaga.
Julai 27, 2022, Paulo alidaiwa kuondoka nyumbani saa nne asubuhi akiongozana na mkewe na kudai wanakwenda kukata masanzu kwa ajili ya kujenga zizi la ng’ombe, kisha wakaelekea msituni, lakini Paulo alirejea nyumbani kwake saa mbili usiku bila mkewe.
Baada ya upekuzi msituni, mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umefunikwa na matawi ya miti na nyasi huku ukiwa na jeraha la kukatwa shingoni na kitambaa kilichokuwa kimeingizwa kwenye mdomo wake.
Hukumu iliyotupilia mbali rufaa ya Paulo kupinga hukumu hiyo ilitolewa jana, Aprili 16, 2026, na jopo la majaji watatu ambao ni Lugano Mwandambo, Abraham Mwampashi na Lameck Mlacha, walioketi Arusha.
Jaji Mlacha alieleza kuwa baada ya kupitia kwa kina ushahidi uliotolewa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha pamoja na hoja za pande zote, Mahakama ya Rufani haikuona sababu ya kuingilia uamuzi wa mahakama ya chini.
Mahakama imesema kuwa mrufani alijaribu kukimbia, jambo lililoashiria kuwa na hatia, na kuwa wakati akihojiwa alikiri kumuua mkewe na kukataa utetezi wake kuwa mkewe aliuawa na fisi.
Awali, Paulo alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Arusha kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.
Ilibainika kuwa Februari 27, 2022, katika eneo la Ngereyani Emboong’eti “A”, Wilaya ya Longido, alimuua mkewe kwa kumkata shingoni kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Katika hatua za awali za kesi, mrufani alikiri kosa hilo, lakini kutokana na uzito wa kosa la mauaji ambalo adhabu yake ni kifo, mahakama iliamua kuendelea kusikiliza ushahidi ili kuthibitisha hatia yake kwa mujibu wa sheria.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi wanane pamoja na vielelezo viwili ambavyo ni ripoti ya uchunguzi wa maiti (postmortem) na ramani ya eneo la tukio.
Kwa upande wake, mrufani alitoa utetezi wake akiwa shahidi pekee bila kuwasilisha kielelezo chochote.
Shahidi wa nne, ambaye ni mama wa mrufani, Naishoka Laizer, alidai siku ya tukio alimwona mwanawe akiondoka nyumbani pamoja na marehemu wakielekea msituni kwa ajili ya kukata masanzu.
Alidai usiku wa siku hiyo mrufani alirejea nyumbani peke yake bila kutoa maelezo yoyote kuhusu alipo marehemu.
Alidai hali hiyo ilizua wasiwasi kwa familia, ambapo aliamua kumtuma mwanawe mwingine aende kumtafuta, ambapo alikutana na shahidi wa tano aliyedai kuwaona mrufani na Ndomononi wakielekea msituni.
Shahidi huyo aliongozana na shahidi wa pili, Supeti Philipo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kijiji, hadi msituni ambapo walikuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa na matawi ya miti na nyasi, na walipoangalia karibu walibaini alikuwa na jeraha la kukatwa shingoni na kipande cha kitambaa mdomoni.
Supeti alidai kumjulisha Mtendaji wa Kijiji, kisha taarifa ikatolewa polisi ambao walienda eneo hilo na kuchukua mwili wa marehemu kuupeleka hospitali.
Ushahidi mwingine uliowasilishwa mahakamani na shahidi wa sita, ambaye ni ndugu wa mrufani, ulidai kuwa siku hiyo, saa 4:45 usiku, Paulo alitoka na walipomuuliza alidai anakwenda sokoni kununua ugoro na sabuni, na alipoulizwa kuwa wauzaji watakuwa wameshaondoka sokoni hakujibu kitu kisha akaondoka.
Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili huo alieleza chanzo cha kifo hicho ni kutokwa na damu nyingi kutokana na jeraha la kukatwa, ambapo mishipa mikubwa ya shingo ilikatwa na kitu chenye ncha kali.
Kwa kuzingatia kuwa Paulo alikuwa mshukiwa na alitoweka nyumbani kwake, msako ulianza, ambapo walilazimika kupanda pikipiki na kufanikiwa kumkamata katika gari alilokuwa amepanda, kisha akapelekwa kituo cha polisi.
Katika utetezi wake, Paulo alikiri kwenda msituni na mkewe lakini akakana kumuua, ambapo alidai walipoingia msituni walivamiwa na kundi la fisi ambalo lilimvuta mkewe msituni, na kuwa alikwenda sokoni kuomba msaada lakini hakupata.
Alidai kuwa alipokuwa akizunguka kijijini akitafuta msaada, gari la polisi lilitokea na kumtia mbaroni kwa tuhuma za mauaji.
Mahakama hiyo ya chini ilikataa utetezi wa mrufani kuwa mkewe aliuawa na fisi, ikieleza kuwa fisi hawakuwa na kitu chenye ncha kali cha kukata shingo ya marehemu, hawakuwa na uwezo wa kuweka kipande cha kitambaa mdomoni kwa marehemu wala kufunika mwili wa marehemu kwa nyasi na matawi ya miti.
Mahakama ilizingatia kuwa mrufani alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa hai, na alishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kilichotokea.
Kutokana na ushahidi huo wa kimazingira, mahakama ilimhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa, uamuzi ambao ulipingwa na mrufani katika Mahakama ya Rufani.
Katika rufaa hiyo, Paulo aliwakilishwa na wakili na alidai kuwa ushahidi haukutosha, mashahidi hawakuaminika, na kwamba utetezi wake haukuzingatiwa ipasavyo.
Upande wa Jamhuri ulipinga rufaa hiyo, ukisisitiza kuwa ushahidi uliowasilishwa ulithibitisha hatia ya mrufani bila kuacha shaka.
Jamhuri ilieleza kuwa mrufani ndiye aliyemuua marehemu kwani alikiri kosa, kama inavyoonekana katika ukurasa wa 23 wa rekodi ya rufaa, na kuwa mahakama ilisikiliza kesi na hatia ya mrufani ilitokana na ushahidi wa kimazingira na kanuni ya mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, ambayo ilithibitishwa ipasavyo.
Jaji Mlacha amesema baada ya kupitia mwenendo na mawasilisho ya pande zote, Mahakama imejiridhisha kuwa Ndomononi alikufa kifo kisicho cha kawaida; mwili wake ulikuwa na jeraha huku ukiwa umefunikwa, na alienda msituni na mumewe akiwa hai.
Amesema kuwa suala ambalo mahakama ililazimika kulishughulikia ni kubaini nani alimuua marehemu, kwani hakuna shahidi hata mmoja wa mashtaka aliyeshuhudia mauaji hayo, hivyo ushahidi uliotumika ni wa mazingira.
Mahakama pia ilirejea kanuni ya kisheria ya “mtu wa mwisho kuonekana na marehemu,” ikisema kuwa pale ambapo mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu, anawajibika kutoa maelezo ya kuridhisha kueleza mazingira ya kifo hicho.
Jaji Mlacha amesema katika kesi hiyo walibaini kuwa maelezo ya mrufani kuhusu shambulio la fisi hayakuwa na mantiki wala ushahidi wa kuunga mkono, na hivyo yalikataliwa ipasavyo na mahakama ya chini.
Aidha, mwenendo wa mrufani baada ya tukio, ikiwemo kushindwa kutoa taarifa kwa familia, kuzunguka kijijini bila kueleza tukio na kujaribu kutoroka, ulionyesha dalili za hatia.
Mahakama ilihitimisha kuwa mnyororo wa ushahidi wa kimazingira ulikuwa kamili na ulimwelekeza moja kwa moja mrufani kama mhusika wa mauaji hayo bila uwezekano wa mtu mwingine.
“Ilikuwa ushahidi wa shahidi wa nne kuwa mrufani alirudi nyumbani saa mbili usiku peke yake, hakuweza kueleza alipo mkewe, na akaamua kwenda sokoni kununua ugoro licha ya kuambiwa muuzaji wa bidhaa hiyo hakuwepo; hatimaye alikiri kosa. Mambo haya hayaendani na kutokuwa na hatia.”
Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa hiyo na kuthibitisha hukumu ya kifo dhidi ya Paulo
