FYATU MFYATUZI: Fyatu akataa PhDi za kisanii na kimagumashi

Juzi, nilipata habari mbaya. Japo kwa mashaka na mstuko, nilipokea habari toka chuo kimoja nakiita choo kikuu toka kaya moja inayosifika kuwa na mafyatu wanaosifika kwa utapeli na uvivu na kupenda dezo hadi wanaaibisha sifa yake na ya bara letu.

Nilibanjiwa kuwa nimepewa, sorry, nimetunukiwa PhDi nyingine ya yada yada yada na upuuzi mwingine mwingi! Bahati mbaya kwao na nzuri kwangu, hawakujua kuwa mie ninazo PhDi tatu za kubukulia na si za kuzawadiwa.

Hivyo siingii mkenge. Hawakujua kuwa nimenyaka PhDis zangu tena orijinali toka vyuo vikuu vinavyokubalika duniani.

Nilipouliza kwa nini wanataka kunizawadia shahada na kunifanya sijapiga buku. Sipendi na kuwa sifa, hakuwa na la maana la kujibu.

Walichofanya bila kufanikiwa ni kunisifiasifia tena kizwazwa kwa utapeli wao wasijue mie siyo mlevi wa sifa uchwara wakati ni mbukuzi wa kupigiwa mfano.

Katika kujitetea, walisema eti walitaka kunizawadia, sijui kunitunuku shahada mawenge eti kwa sababu eti wasomi wa huko, wawe wa kweli au uchwara, wangegundua kuwa nina akili kuliko viumbe wote angani na ardhini.

Wamenipamba hadi nikaonekana kama ka muungu fulani wakidhani nitaingizwa cha kike kirahisi kumbaff hawa waliodhani nami ni mkubaff kama wao au mpenda sifa wanitumie.

Kunogesha mambo eti wanadai kuwa walikuwa wakinifuatilia, kunisikiliza, na kunisukuti mie bila kujua! Walidai kuwa wanahusudu uwezo wangu wa kufyatuka na kufanya maamuzi.

Niliwauliza kama weshamtunuku munene wa kaya yao. Hawakuwa na la kujibu. Hawakujua kuwa mojawapo ya uamuzi wangu ni kukataa utapeli na uzwazwa wao. Kabla hata ya kujua nini kingeendelea na ukumbafu wao, niliwauliza. Je, hii ni nini wanipende wakati siwajui na wala sijawahi kuwafanyia lolote zaidi ya kujihusisha na mafyatu wangu kama siyo udaku na udukuzi? Hawakuwa na la maana la kujibu. Niliwaambia point blank.

Sasa nawaonya hawa matapeli na wengine wote wanaotaka kutumia unene wangu kuniingiza mkenge. Kwanini mnamsikiliza fyatu bila kujua ili mmtumie siyo? Mmenoa kwangu. Nenda kwa vihiyo na vilaza wanaoshobokea huu upuuzi walioogopa umande. Mie nimepiga buku bwana. Kutaka kunitwisha mkenge, wanadai eti waligundua kuwa baada ya kuumbwa kwa Yesu Alayhi s-salām, yule mwana wa Maria na Mungu na mtume Muhammad all -llāhu alayhī wa-sallam wa’ala alihi wa sahbihi hakuna kiumbe mwingine bora aliyeumbwa isipokuwa mimi.

Ya kweli au kamba za kutaka kuniingiza cha kike? Nilishangaa.

Je, kwa nini mimi? Katika kufanya utafiti wa haraka, nilistuka. Nliwatumia baruapepe yenye mapepe tena kwa mapepe. Niliuliza kama walishawahi kumtunukia hiyo shahada kwa munene wa kaya yao.

Ukiachia mbali mimi kuwa munene mwenye akili nyingi kuliko wote aliwahi kuumba wadudi, ni chaguo la Mungu. Maana, bila Mungu kukuchagua, huwezi kuwa kiongozi.

Najua. Wapo wanoko wanaohoji unene wangu. Nawambia wapende juu wakazibe. Wapo wanaohoji usomi wangu. Waniambie wao wametunukiwa PhDi ngapi kama wana ubavu. Najua wapo wanaoniona kihiyo.

Maskini hawajui kuwa bila kuwa zinachemka sana na kwelikweli hata uwe nani, huwezi kutunikiwa shahada ya heshima ndo maana nimepewa.

Hawajui kuwa shahada ya heshima ina maanisha kuwa una akili zinazoheshimika kuliko za wasomi wote duniani.

Lazima wajue. Ebo, kama wapo wanaojiona wamesoma sana, wajiulize. Nateua wasomi wangapi tena ambao wananinyenyekea na kuimba sifa zangu? Kwani, usomi ni dili au dili ni unene?

Tokana na akili zinazochemka kuliko viumbe wote, ujanja, ujuzi, na vipaji vya ajabu, nina shahada za heshima karibu katika kila nyanja.

Nina shahada za utunzaji wadudu hasa chawa, amani, kutunza uhai wa mafyatu, matumizi mazuri ya njuluku zao, kudumisha amani na mshikamano, kutunza maadili na kupiga madili sorry, kulinda raslimali za mafyatu na mengine mengi kama hayo.

Katika kusukuti, kwa kutumia usomi na ugwiji wangu niligundua kuwa kumbe kuna vyuo aka vyoo vikuu kanjanja ambayo hutoa shahada kama hizi kwa wanene ili wawe karibu nao wapate lau njuluku au upendeleo. Hawakawii kukutumia kadi za kuomba mchango na kukugeuza buzi la kuchunwa. Wengine wanaweza kukupa shahada bomu kama nyenzo ya kukutumia kutangaza utapeli wao kwa wanene wengine vihiyo na wasiofikiria ili kupata upendeleo au kuwatumia kupiga njuluku kwa kuwaingiza wanene wengine mkenge. Nimestuka.

Niliwapa wazi kuwa siko tayari kupokea shahada mawenge kwa sababu mie ni doktari tena mwenye PhDii lukuki zote za kubukua. Kwa wasiojua shahada za heshima zisizo na heshima, ni janja ya makanjanja na matapeli ya kuwanasa wanene vihiyo na vilaza walioogopa umande. Wakishaukwaa mkenge au kujiingiza kwa kuzinunua kutaka ujiko wa kuitwa au kuonekana wasomi, utawasikia waimba kwaya na wapambe wao wakiwaita hata kuapongeza kwa ujinga huu. Wapo wengi wanaowaingiza mkenge kwa kuwaita maprofesa Emerita, sorry, emeritus bila kujuua hata maana yake. Nashauri wanene tuogope shahada hizi uchwara zisizo na heshima.

Mwisho, natangaza rasmi. Ieleweke. Sitaki shahada uchwara. Nimepiga shule bwana. Du! Kumbe tulilala mlango wazi!