Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kukusanya ushahidi wa taarifa ya Hilda Newton aliyoichapisha na kusambaza katika mitandao ya kijamii akidai Serikali kupanga kumuua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Tundu Lissu.
Wakati uchunguzi huo ukiendelea polisi imemtaka Hilda kufika ofisi ya mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Dar es Salaam, kutoa ushahidi wa madai hayo, hata hivyo, mwenyewe amejibu kuwa anasubiria wito rasmi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Aprili 22, 2026 na Msemaji wa Polisi, David Misime inaeleza kuwa, Hilda alichapisha taarifa Aprili 10, 2026.
Kwa mujibu wa Misime, taarifa hiyo ya Hilda inaeleza kuwa, pamoja na mambo mengine Serikall imepanga kumuua Lissu (Mwenyekiti wa Chadema) kwa risasi.
“Ili kukamilisha uchunguzi Jeshi la Polisi linamwelekeza Hilda kufika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, iliyopo katika jengo la makao makuu ndogo ya polisi iliyopo Dar es Salaam Aprili 24, saa nne asubuhi ili kuwasilisha ushahidi aliosema na kuutangazia umma kuwa anao.
“Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 11 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023,” amesema Misime katika taarifa hiyo.
Akizungumza na Mwananchi Hilda amesema,“nani alisema ushahidi unatolewa polisi? Kingine waniletee wito rasmi, wanajua pakunipata, si kipindi kile walivyonikamata walichukua details (vielelezo) zangu, wanajua pakunipata,” amesisitiza Hilda.
Wakati hayo yakiendelea, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa ameshauri kufuatia suala hilo, atafutwe Hilda aliyetoa madai hayo kama ambavyo taarifa ya polisi ilivyoanisha.
“Taarifa hii inamhusu Hilda na amepewa wito, itakuwa vyema na sahihi atafutwe yeye ili kuzungumzia jambo hili. Sisi tuna wasiwasi na afya kama ambavyo ndugu zake walivyowahi kutujulisha kutokana na vyuma alivyonavyo mwilini kumuwasha,” ameeleza Golugwa wakati akizungumza na Mwananchi.
