Shahidi aeleza jinsi ofisa mtendaji wa kata alivyohusika kumuua mkewe

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa jinsi Dominic Mushi anavyodaiwa kutekeleza mauaji ya mkewe, Diana Hugo, kwa kumnyonga hadi kufa, kisha kuufunika mwili wake kwa shuka na kuulaza kifudifudi kitandani, huku pembeni ya mwili huo kukiwa na chupa moja ya K-vant na kikombe cha plastiki cha rangi ya bluu.

Diana, ambaye alikuwa mfanyakazi wa benki ya NMB tawi la Airport, anadaiwa kuuawa na mumewe na mwili wake ulikutwa kitandani ukitoka damu puani, masikioni na mdomoni.

Mushi, ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Gongo la Mboto na mkazi wa Kinyerezi, anakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya mkewe Diana, tukio analodaiwa kulitenda Oktoba 14, 2024 katika eneo la Kinyerezi Kichangani, Wilaya ya Ilala.

Hata hivyo, katika maelezo yake ya onyo aliyoyatoa Kituo cha Polisi Stakishari, mshtakiwa huyo alidai hajui chochote kuhusiana na tukio la kifo cha mkewe. Badala yake, alidai kuwa kelele za kuomba msaada alizokuwa akizipiga mkewe usiku huo zilikuwa ni ndoto aliyokuwa anaota.

Hayo yameelezwa jana, Jumanne Aprili 21, 2025, na askari Polisi mwenye namba J 428, Ditektivu Koplo Daniel kutoka Kituo cha Polisi Stakishari.

Daniel alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, aliyepewa mamlaka ya nyongeza kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Mshtakiwa Dominic Mushi anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mke wake, Diana Hugo. Akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Koplo Daniel alidai kuwa yeye ndiye aliyekuwa mpelelezi katika kesi hiyo na ndiye aliyemfanyia mahojiano na kuandika maelezo ya onyo Oktoba 29, 2024.

Akihojiwa na jopo la mawakili wawili wa Serikali, Brenda Massawe na Hakme Pembeni, alidai kuwa Oktoba 14, 2024 aliitwa na mkuu wake wa kazi, SP Albogasti Kilulumo, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Ukonga, na kuambiwa aandae vifaa kwa ajili ya kwenda eneo la tukio la mauaji Kinyerezi Kichangani.

Aliandaa vifaa akishirikiana na askari wenzake, kisha waliondoka kwenda Kinyerezi hadi katika nyumba (apartment) aliyokuwa akiishi Mushi na mkewe Diana.

“Katika eneo lile kuna nyumba sita. Tulipofika, tulikuta geti limefungwa, hivyo tuliingia kwa kutumia gari la pili na kukuta kundi la watu nje ya uzio wa nyumba hiyo,” alidai Daniel, ambaye ana uzoefu wa miaka kumi kazini.

Daniel, shahidi wa 10 wa Jamhuri, alidai kuwa baada ya kuingia ndani ya uzio, Mkuu wa Upelelezi alijitambulisha kwa kundi hilo la watu, kisha alitokea mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Sudi Abdallah.

Sudi aliwaeleza kuwa yeye ndiye aliyeachiwa funguo ya nyumba, kisha akawafungulia mlango ili askari hao waingie ndani kwa ukaguzi.

“Ndani ya nyumba ya Mushi kulikuwa na vyumba viwili na sebule. Sebuleni kulikuwa na sofa na televisheni. Pembeni kulikuwa na chumba kimoja kinachoonekana hakitumiki, na kingine ndipo tulikuta mwili wa Diana ukiwa umelala kifudifudi,” alidai shahidi.

“Katika chumba hicho tulikuta mwili wa marehemu Diana kitandani ukiwa umefunikwa na shuka, lakini miguu na kichwa vilikuwa wazi. Maeneo ya masikio, pua na mdomo yalikuwa yanatoka damu,” aliongeza.

Mshtakiwa Dominic Mushi anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mke wake, Diana Hugo. Akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Aliendelea kudai kuwa pembeni ya mwili huo kulikuwa na kikombe cha plastiki cha rangi ya bluu chenye vitu vyeupe vilivyoganda, pamoja na chupa ya kinywaji aina ya K-vant na karatasi za dawa zinazoonyesha kuwa zimetumika.

“Nilimuita askari waliokuwa nje wakiimarisha ulinzi ili kusaidiana kuubeba mwili na kuuweka kwenye gari, kisha tuliupeleka kuuhifadhi katika Hospitali ya Polisi Kilwa Road kwa hatua zaidi, ikiwemo uchunguzi,” alidai Daniel.

Baada ya kupeleka mwili hospitalini, Koplo Daniel na mkuu wake walienda zahanati ya Kinyerezi ambapo mtuhumiwa alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

“Tulikuta daktari anaendelea kumpa matibabu huku Mushi akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Baada ya hapo tulirudi kituoni, na nilipewa jalada la kesi ya mauaji kwa ajili ya kuendelea na upelelezi,” alidai.

Baada ya kupokea jalada hilo, alianza uchunguzi kwa kumhoji Sudi Abdallah, mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kichangani, na kupata maelezo ya ziada.

Pia alipata maelezo kutoka kwa Josephat Silunga, mlinzi wa eneo hilo, pamoja na majirani akiwemo Hamisi na mke wake.

Alidai kuwa nyumba hiyo ilikuwa na wapangaji sita, wote wakiwa wanaishi kama wanandoa.

Aliongeza kuwa Oktoba 16, 2024 alipokea maelekezo kutoka kwa Inspekta Kweka kuwa ndugu wa Diana walifika kituoni kwa ajili ya kufanya utambuzi wa mwili.

“Tuliongozana nao hadi Hospitali ya Kilwa Road, ambapo Inspekta Kweka na ndugu wawili wa marehemu waliingia chumba cha uchunguzi. Tulichukua maelezo yao na kuwakabidhi mwili, kisha tukarudi kituoni,” alidai.

Hata hivyo, shahidi huyo alidai kuwa ripoti ya daktari ilieleza kuwa Diana alifariki dunia baada ya kukabwa shingo na kukosa pumzi.

“Oktoba 18, 2024 nilipata maelezo ya Samsoni aliyesema aliombwa msaada na mlinzi wa eneo hilo siku ya tukio,” alidai.

Pia alieleza hali aliyoikuta nyumbani kwa Dominic Mushi, akidai kulikuwa na kelele za kuomba msaada.

Hata hivyo, Oktoba 29, 2024 Dominic Mushi alipelekwa Kituo cha Polisi Stakishari akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Nilimhoji mshtakiwa kwa maelezo ya onyo, ambapo alieleza kuhusu ndoa yake na Diana, lakini kuhusu tukio la mauaji alisema hajui chochote na kuwa mkewe alikuwa anaota siku hiyo,” alidai shahidi.

Baada ya mahojiano, mshtakiwa alisoma maelezo yake na kusaini.

Alipoulizwa aligundua nini katika upelelezi wake, shahidi alidai aligundua kuwa mtuhumiwa ndiye anayehusika na mauaji hayo kwa kuwa waliishi pamoja na siku ya tukio walikuwa ndani, huku mlango ukiwa umefungwa kwa ndani.

“Pia maelezo ya mashahidi yalinithibitishia kuwa Dominic ndiye aliyemuua Diana,” alidai.

Aliongeza kuwa ushahidi wa daktari, mashahidi na mazingira unaonyesha kuwa Dominic ndiye mhusika, kwani kifo cha Diana kilitokana na kukabwa shingo na kukosa pumzi.

“Kulingana na maelezo ya mashahidi na upelelezi wangu, Diana alikuwa akiishi na mumewe Dominic katika moja ya nyumba (apartment) zinazomilikiwa na Elisha Emmanuel,” alidai.

Hata hivyo, shahidi alimtambua mshtakiwa mahakamani. Mshtakiwa anatetewa na wakili Roman Lamwai, na kesi hiyo imeahirishwa hadi leo mchana, ambapo shahidi wa 11 wa upande wa mashtaka ataendelea kutoa ushahidi.