ALIYEKUWA kamishna wa makocha wa Shirikisho la Mpira Kikapu nchini (TBF), Robert Manyerere amesema bila uwekezaji, ni ngumu kwa timu za Tanzania kufanya vizuri kimataifa.
Manyerere aliliambia Mwanaspoti baadhi ya timu za nje zilizoshiriki Ligi ya Afrika (BAL) zimefanya uwekezaji mkubwa na kuwa tishio kwenye mchezo huo.
Aliitaja Dar City iliyoshiriki pia ligi hiyo ni moja ya timu zilizofanya uwekezaji kwa kusajili wachezaji kutoka nje na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo kufika robo fainali ya BAL.
“Timu hii ndiyo inayoweza ikatoa ushindani katika mashindano ya kimataifa,” amesema Manyerere na kuongeza, pia imeitangaza Tanzania kimataifa kwa kushiriki katika michuano hiyo kuanzia Road to BAL Elite 16 iliyofanyika Kenya.
Pia aliitaja Stein Warriors imefanya uwekezaji kwa kusajili wachezaji wazawa wenye uwezo na timu zinazosimamiwa na taasisi kama ABC, JKT, Jeshi Stars na JKT Stars, zinafanya vizuri huku pia kukiwa na zile zinazoendeshwa kutokana na michango ya wanachama.
Kwa upande wake, kocha Kassimu Jumbe kutoka Kinondoni amesema bila ya uwekezaji kwa timu nyingine, zitaishuhudia Dar City pekee ikishiriki kimataifa.
Timu za Tanzania zilizowahi kushiriki mashindano ya BAL, ni JKT, ABC na Kurasini Heat na zilishindwa mapema kutokana na kutokuwa na wachezaji wenye viwango vikubwa, huku Kurasini ikipata nafasi ya kushiriki Road to BAL Elite 16 (2022) iliyofanyika Afrika Kusini, lakini ilishindwa kutokana na kukosa fedha za maandalizi.
