Zaidi ya kaya 1,000 Makambako hazina vyoo bora

Njombe. Zaidi ya kaya 1,132 katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe zimetajwa kukosa vyoo bora, hali ambayo inayohatarisha usalama wa afya za wananchi kutokana na uwezekano wa kupata magonjwa ya mlipuko kiurahisi.

Hayo yamesemwa leo Aprili 14, 2026 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Kenneth Haule wakati akipokea taarifa ya usimamizi shirikishi wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira katika kikao kazi kilichofanyika Makambako mkoani Njombe.

Amesema Kata ya Lyamkena inatajwa kuwa kinara kwa kutokuwa na vyoo bora ambapo kaya 418 zimekosa vyoo, hivyo ndani ya halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

“Kijiji cha Mtulingala kilichopo kata ya Kitandililo kina kaya 313 na kaya zaidi ya 254 hazina vyoo kabisa, nyingine zipo katika Mtaa wa Kilimahewa, Ibumila, Idofi, Malombwe, Kiumba na Makatani,” amesema Haule.

Amewataka viongozi wa serikali za mitaa na vijiji kuhakikisha kuwa kila kaya ndani ya halmashauri hiyo inakuwa na choo bora na kuwa na maji tiririka ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

‎Ofisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Neema Shuaka amesema ili kujenga choo bora inatakiwa kuzingatia kanuni za msingi na sifa kuu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

“Sifa hizo ni kuwa na ukuta imara unaosafishika, sakafu inayosafishika, paa ambalo halivuji, mlango unaofunguka na kufunga, bomba la kutolea hewa nje na kifaa cha maji tiririka na sabuni ya kunawia mikono.

‎Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kahawa, Daudi Mwamlima amewataka watendaji wa serikali kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuhakikisha hawafumbii macho suala la usafi wa mazingira.

“Tunaahidi kuhakikisha kila kaya inajenga choo bora lakini watendaji wa serikali wasifumbie macho suala la usafi wa mazingira kwa ujumla,” amesema Mwamlima.