FYATU MFYATUZI: Fyatu sasa kutopokea mshahara tena japo….

Baada ya vyuma kukaza kutokana na ufyatu na wendawazimu wa Donnie Tarampu na Ben Niitenyau, Fyatu natangaza rasmi kuwajibika. Kuanzia leo, sitapokea mshahara wangu. Je, ni kiasi gani? Siwaambii. Niwambie mje mniibie? Mmenoa ile mbaya. Naona yule anatoatoa mimacho akipekua gazeti kutaka kujua nanyaka mabilioni mangapi ya madafu.

Ukome na ukomoe kabla sijakukomoa na kukomesha kama kupanda kwa gharama za maisha. Chichemi. Mshahara wangu. Ni chiri kubwa njomba tena kwa ajili ya usalama wa kaya. Ila niaminini hata kama ni kamba, sorry, makakati au siyo.

Hata hivyo, kwa namna ninavyoishi ubwete, sikupaswa kulipwa mshahara. Mshahara wa nini wakati niliomba mwenyewe kuwatumikia mafyatu ambao huwatumia na kunitumikia badala ya kuwatumikia?

Kwanza, nilikuwa napokea mshahara mkubwa bila ulazima tena kwa kutofanya kazi au kufanya kazi rahisi. Sikuwa naulipia au kukatwa kodi. Nitakatwaje kodi wakati mie ndiyo mmilki wa kila kitu ikiwamo Fyatuland kwa mujibu wa katiba? Hivyo, roho imenifyatua nikaamua kutopokea mshahara kabisa kuanzia sasa.

Pili, naishi, kula, kulala, kutanua, kujienjoy, na kutibiwa tena ughaibuni bure. Nasafiri tena kwa pipa bure. Natumia nitakavyo bila kuulizwa wala kuzuiliwa wala kukaguliwa.

Isitoshe, siyo mimi pekee anayetumia ubwete. Hata vitegemezi na maswahiba zangu wanatumia ubwete. Tokana na vyuma kukaza, itabidi wasahau japo kwa muda. Walizoea kutesa. Ngoja nao wateseke kama Mafyatu wanaowafyatua kila uchao.

Tatu, natanua nitakavyo na wakati na namna nitakavyo. Nikijisikia kuchoka mikelele ya Mafyatu, huwa nakwenda zangu majuu kuning’inia kama jamaa yangu Njaa Kaya alivyofanya kule Ubrazil na kidosho wake miaka mile ya uvasco da gama au mmesahau? Jamaa alikuwa wa hovyo na mbinafsi tena mpenda matanusi. Haijawahi kutokea. Naomba isiotokee tena.

Nne, sihitaji mshahara. Wa nini wakati nilizokwishapiga ni nyingi na za kutosha kuendesha maisha ya hata Mafyatu elfu moja kwa miaka elfu kumi. Nikikaa, nalipwa. Nikisimama, nalipwa. Nikipayuka au kufyatua, nalipwa. Nikiota, nalipwa. Ni kulipwa, kulipwa, na kulipwa bila mwisho.

Nalipwa hadi nachukia. Halafu unaona mifyatu mivivu ikifyatuka na kupayuka eti vyuma vimekaza. Mnataka visikaze siyo? Chakarikeni. Pigeni dili kama vile kuwa wanasiasa au wahubiri wachunaji muone. Unawapa maneno Mafyatu, unaongoka na njuluku laini.

Kwani, sisi wanasiasa na wahubiri, zaidi ya maneno, huwa tunawapa nini Mafyatu tuwafyatuao kila uchao? Kama kawa, wote hutoa ahadi hewa na zisizotekelezeka, na Mafyatu kwa uzwazwa wao huzipokea na kutuamini wakati hatuaminiki japo tunajiamini kwenye upigaji huu rahisi?

Tano, kuanzia sasa, nitakuwa nakwenda mzigoni ima kwa baiskeli au bajaji ikizidi. Tokana na kutopata muda wa kufanya mazoezi na kuongeza uzito, siku nyingine, nitakwenda kwa mguu lau nikumbuke zama zangu za utoto nikienda skuli pekupeku. Naona lile linashangalia. Unadhani nitapita mitaani kwenu mnifyatue? Ng’o. Hamnipati mnifanyie kitu mbaya. Wasiojulikana mlie tu. Hata viyoyozi home na kwenye mchuma nitavizima ili kupunguza matumizi.

Sita, kuanzia sasa, wanene wote wanapaswa kupunguzwa mishahara, magari, wafanyakazi wa ubwete kama vile madereva, wapishi, watunza bustani, walinzi, mabaunsa, mashavu, viribatumbo nk. Pia, nitaanza kuwapeleleza.

Nataka kujua wenye nyumba ndogo. Hapa, ima waziachie au waachie ngazi. Kwanini kuwa na nyumba ndogo wakati wana nyumba kubwa? Huu, naamini. Utakuwa ukombozi kwa akina mama. Akina mama hoyeee! Nyumba ndogo ziii! Mnaotegemea kuchuna mabuzi mtakoma usawa huu. Nitahakikisha mnaisha nawatoa peponi mlioko ili muishi motoni. Wala sitanii. Mjue.

Saba, kuanzia sasa, naanza kukagua matumbo ya wanene niliowateua wakiwa wamekonda. Sasa, naona wengine wamenepeana hata makalio. Kama una kiribatumbo, au masaburi manene, nakufyatua hata unipambe na kunisifia vipi. Badili ya Mafyatu kupanua bongo, wanapanua miili. Maana, ni ushahidi kuwa unawafyatua mafyatu na njuluku zao. Hivyo, wenye viribatumbo jiandaeni kuvipunguza kabla sijawapunguza.

Nane, mikutano, semina, na makongamano ya upigaji na ufyatuaji vya mchongomchongo mwisho wake sasa. Hakuna vitu kama hivi wakati huu ambapo vyuma vimekaza. Lazima nami ni wakaze hadi wajikaze na kupunguza kukaza kwa vyuma. Si inapendeza?

Tisa, nimekuja na kamba, sorry, na mkakati huu kuonyesha ninavyowajali Mafyatu. Hivyo, nategemea wataandamana kunipongeza kwa kuonyesha mfano na upendo visivyowahi kuwepo duniani.

Hii, pia, inaonyeshe nisivyo mbinafsi wala msaka ngawira kama wengine wanwafyatuao na kuwanyonya Mafyatu wao kupitia mgongo wa unene.

Kumi, kuanzia sasa, wote ambao wameendelea kuficha ukwasi wao nawapiga kalamu. Haiwezekani Mafyatu waendelee kusota na kufunga mikanda huku walaji wakitesa na kupanua matumbo na mikanda.

Hii si haki hata kidogo. Kwa vile nimepata roho mtakatifu aliyemfukuza roho mtakakitu aliyekuwa amenitawala kwa miaka mingi, mtegemee mengi.

Ama kweli, yajoyo yanafurahisha. Hivi, sasa hivi ni saa ngapi, siku gani na niko wapi?