Zanzibar. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imezindua rasmi Jukwaa la The Citizen Rising Woman visiwani Zanzibar, ikiweka msisitizo kuwa uwezeshaji wa wanawake si suala la kijamii pekee bali ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa.
MCL wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen, MwanaSpoti na majukwaa mbalimbali ya mitandaoni wamezindua jukwaa hilo leo usiku Aprili 15, 2025.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na watu mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayochochea ushiriki wa wanawake katika maendeleo ya Taifa.
Amesema kwa zaidi ya miaka sita, jukwaa hilo limekuwa likifanyika Tanzania Bara, lakini sasa limepelekwa Zanzibar ili kuhakikisha wanawake wanakuwa sehemu ya majukwaa makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimkakati.
“Ukuaji wa Taifa hauwezi kukamilika bila Zanzibar kuwa kitovu cha mijadala na uwekezaji unaowahusisha wanawake,” amesema Rosalynn.
Mkurugenzi huyo amesema kupelekwa kwa jukwaa hilo Zanzibar si mwendelezo wa kawaida, bali ni uamuzi wa makusudi wa kupanua wigo wa uwezeshaji wanawake nchini.
Amesema jukwaa la Rising Woman limebadilika kutoka tukio la siku moja na kuwa mfumo mpana unaojumuisha kuunganisha wadau, kukuza uongozi wa wanawake na kuchochea uwekezaji unaowalenga wanawake.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Give to Gain” (Toa ili Upate), Mkurugenzi huyo amesema falsafa hiyo inaelekeza namna uwekezaji kwa wanawake unavyoweza kuzaa matokeo chanya.
Amebainisha utoaji wa fursa huzaa ubunifu, utoaji wa mtaji hujenga biashara zenye tija, huku utoaji wa nafasi na mwonekano ukizalisha kizazi kipya cha viongozi wanawake.
“Hii si ajenda ya kijamii pekee, ni mkakati wa kukuza uchumi,” amesema Rosalynn.
Akizungumzia fursa zilizopo visiwani humo, Mkurugenzi huyo amesema Zanzibar ina nafasi kubwa katika uchumi wa bluu na utalii, lakini mafanikio hayo yatategemea ushiriki wa wanawake.
Amesisitiza wanawake wakipewa mitaji, masoko na nafasi za uongozi, Zanzibar inaweza kuwa mfano wa ukuaji jumuishi si kwa Tanzania tu, bali Afrika na dunia kwa ujumla.
“Uwezeshaji wa wanawake si hisani, ni uwekezaji wenye faida. Mwanamke anapoinuka, jamii nzima inanufaika,” amesema Rosalynn.
Wito umetolewa kwa viongozi wa bodi na wamiliki wa biashara nchini kutambua kuwekeza kwa mwanamke si suala la hisani, bali ni mkakati wa kibiashara wenye tija unaoweza kuimarisha taasisi na kukuza uchumi wa Taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, David Nchimbi, amesema ushahidi wa kimataifa unaonyesha kampuni zenye uwakilishi mkubwa wa wanawake katika ngazi za juu za uamuzi hupata mafanikio makubwa zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, David Nchimbi.
Amesema ni kwa kuzingatia mtazamo huo ndipo bodi ya MCL ilifanya uamuzi wa kumteua Rosalynn Mndolwa Mworia kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza mwanamke katika historia ya kampuni hiyo, akieleza hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani na ufanisi.
“Kuamini katika uongozi wa mwanamke si jambo la hisani, bali ni akili ya biashara inayolenga matokeo chanya na endelevu,” amesema Nchimbi.
Katika hatua nyingine, Nchimbi ameeleza nguvu ya vyombo vya habari ndiyo injini inayotumika kuliwezesha Taifa, akisisitiza ili kufanikisha hilo, taasisi lazima ziwe na uwezo wa kuzungumza na jamii kwa upana wake.
Amebainisha MCL imeendelea kuwa kinara wa ushawishi wa habari nchini kwa kufikia zaidi ya wasomaji milioni 9 kupitia Mwananchi, milioni 2.4 kupitia Mwanaspoti na zaidi ya 580,000 kupitia The Citizen.
Aidha, katika majukwaa ya kidijitali, kampuni hiyo inafikia zaidi ya watu milioni 25 kila mwezi.
Nchimbi amesema wigo huo mpana umeiwezesha MCL kuendesha kwa ufanisi jukwaa la Rising Woman, ambalo katika kipindi cha miaka sita limefanikiwa kutambua na kusimulia hadithi za wanawake zaidi ya 350 walioleta mabadiliko katika sekta mbalimbali.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu ya “Give to Gain”, amesema inalenga kuhamasisha utoaji kama njia ya mafanikio, huku ikiimarisha dhana ya ujumuishi na usawa katika taasisi.
Amesema katika ngazi ya bodi, ujumuishi unasaidia kupata mitazamo mipya inayoboresha maamuzi, wakati usawa unahakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki ya kushiriki katika maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan amesema kazi kubwa imekuwa ikifanyika kuhakikisha wanawake wanawezeshwa kiuchumi.
“Asilimia 65 ya wafanyakazi ZEEA ni wanawake, kwenye uongozi wa juu pia wapo kwa asilimia 80, hii inaonesha wanawake wanaweza kabla ya kuwezeshwa.
“Tumeweza kutoa mikopo kwa wajasiriamali, kuwapa mafunzo, kuwatafutia masoko endelevu na kuwajengea mbinu zitakazowawezesha kufanya biashara kwa urahisi,” amesema.
Burhan amebainisha kuanzia mwaka 2022 hadi Machi 30, 2026, ZEEA imetoa mikopo ya Sh53.9 bilioni ambazo kati ya hizo asilimia 69 imekwenda kwa wanawake.
“SMZ imeendana na kauli mbiu ya Give to Gain, tulitoa hiyo mikopo na wanawake wamekuwa warejeshaji wazuri wa mikopo. Niwapongeze kwa hili wameichangamkia mno fursa ya mikopo,” amesema Burhan.
