Papa Leo Awashambulia “Madikteta” Wanaotumia Mabilioni Kwenye Vita, Atoa Wito wa Amani

Global Publishers
April 17, 2026
0 Comments

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Pope Leo XIV, ametoa kauli kali akiwakosoa viongozi wa dunia wanaotumia mabilioni ya fedha kuendesha vita badala ya kuwekeza katika maendeleo ya watu.

Akizungumza katika mji wa Bamenda nchini Cameroon, Papa Leo alisema dunia inakabiliwa na tatizo kubwa la vipaumbele, ambapo fedha nyingi zinatumika katika uharibifu badala ya kujenga upya jamii.

Alionya pia dhidi ya tabia ya baadhi ya viongozi kutumia dini vibaya kwa maslahi yao ya kisiasa na kijeshi. “Wapo wanaolitumia jina la Mungu na dini kuhalalisha vita na vurugu,” alisema, akisisitiza kuwa imani haipaswi kuwa chombo cha migogoro.

Papa huyo alitembelea eneo hilo ambalo limekumbwa na migogoro kwa karibu muongo mmoja, akisema lengo lake ni kuhubiri amani. Hata hivyo, aligusia kuwa alikuta wananchi tayari wanahubiri amani kwa vitendo.

Katika hotuba yake, alisisitiza athari kubwa za vita kwa binadamu akisema: “Inachukua muda mfupi sana kuharibu, lakini inaweza kuchukua maisha yote kurekebisha.” Aliongeza kuwa mabilioni ya fedha yanatumika kwenye silaha huku sekta muhimu kama afya, elimu na ujenzi wa jamii zikikosa rasilimali.

Papa Leo XIV alitoa wito wa mabadiliko makubwa ya mwelekeo duniani, akihimiza mataifa kuchagua njia ya amani, mshikamano na ubinadamu.

Licha ya changamoto zilizopo, alitoa ujumbe wa matumaini akisema dunia haishikiliwi na “madikteta wachache” pekee, bali pia na watu wengi wenye nia njema wanaoendelea kuijenga kwa mshikamano na upendo.