Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha huduma za kibingwa na kuongeza upatikanaji wa matibabu ya kuokoa maisha.
Akifungua mkutano wa pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya za Upasuaji wa Ubongo Duniani (WFNS), jana Aprili 16,2026, Rais Samia alisema Tanzania imeongeza idadi ya hospitali zinazotoa huduma za upasuaji wa ubongo kutoka mbili zilizokuwepo miaka mitano iliyopita hadi saba kwa sasa.
Alisema hatua hiyo ni matokeo ya uwekezaji endelevu katika miundombinu ya afya na huduma za kibingwa, ukilenga kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hizo ndani ya nchi bila kulazimika kusafiri nje.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alibainisha ongezeko kubwa la wataalamu wa afya nchini, akisema idadi ya wataalamu wa tiba katika nyanja mbalimbali imepanda kutoka 138 mwaka 2020 hadi 1,518 mwaka 2026.
Kwa upande wa wataalamu wa upasuaji wa ubongo (neurosurgeons), alisema wameongezeka kutoka 12 hadi 37, ambapo saba kati yao ni wanawake ishara ya ongezeko la ushiriki wa wanawake katika fani za kitabibu zilizokuwa zikichukuliwa kuwa ngumu na za kiufundi zaidi.
“Mafanikio haya yanaonesha dhamira yetu ya kuimarisha uwezo wa kitaifa na kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi wote,” alisema Rais Samia.
Aidha, alieleza kuwa serikali inaendelea kuboresha mifumo ya afya kupitia mpango wa bima ya afya kwa wote, ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, pamoja na matumizi ya mifumo ya afya ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na uendelevu wa huduma.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya duniani katika kukabiliana na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya vipaumbele vya kimataifa, pamoja na maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Rais alitunukiwa tuzo maalumu ya ubinadamu ya upasuaji wa ubongo kutokana na mchango wake katika kuimarisha huduma za afya na hususan upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu nchini.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, unaotarajiwa kuibua mapendekezo ya kuboresha huduma za dharura, kinga na matibabu ya haraka, sambamba na kuimarisha mtandao wa wataalamu barani Afrika.
Akikabidhi tuzo hiyo, Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Tanzania, Dk Othman Kiloloma, alisema uongozi wa Rais Samia umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, hasa katika kuokoa maisha ya wagonjwa wa magonjwa ya ubongo na uti wa mgongo.
Alibainisha kuwa Tanzania imeongeza uwezo wa kukabiliana na magonjwa hatarishi ya ubongo na uti wa mgongo kupitia uwekezaji wa rasilimali watu, miundombinu na teknolojia.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alisema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika vituo vya kisasa vya tiba kama Kituo cha Sayansi ya Mishipa ya Fahamu cha Mloganzila, upanuzi wa huduma katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), pamoja na kuanzishwa kwa teknolojia za kisasa za uchunguzi na vituo vya urekebishaji.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya majeraha ya ubongo husababishwa na ajali, hususan za bodaboda, ambapo kati ya watu 10 wanaopata ajali, takriban watatu hupata ulemavu wa kudumu.
Magonjwa yasiyoambukiza kama kiharusi, kifafa, maumivu sugu ya kichwa, magonjwa ya neva kwa watoto, maambukizi ya mfumo wa neva, maambukizi ya ubongo na magonjwa ya neva yanayotokana na ajali yametajwa pia kuchangia idadi kubwa ya wagonjwa.
Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) ndiyo kitovu cha tiba za mishipa ya fahamu na ubongo. Katika kipindi cha mwaka 2025 pekee, ilihudumia jumla ya wagonjwa 180,000, ambapo kati yao wagonjwa 10,000 walipata huduma za kibobezi.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025–2026, MOI imekuwa moja ya vituo vya afya vyenye idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa rufaa nchini, wengi wao wakiwa waathirika wa ajali za barabarani, hasa bodaboda, pamoja na majeraha mengine ya mifupa na ubongo.
MOI inahudumia wastani wa wagonjwa 700 kwa mwezi, ambapo takribani asilimia 60 wanatokana na ajali za bodaboda. Hii inaashiria ukubwa wa tatizo hilo katika sekta ya afya.
Takwimu zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya wagonjwa hao hutokana na ajali huku utafiti ukionyesha kuwa chanzo kikuu cha ajali hizo ni mwendo kasi (asilimia 63), uzembe wa madereva (asilimia 58) pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara (asilimia 51). Pia, ukosefu wa elimu ya usalama barabarani umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa.
Akifafanua zaidi Rais Samia alieleza kuwa ziara yake ya mwaka 2022 katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) ilimtoa machozi baada ya kushuhudia hali ngumu ya wagonjwa wa saratani ambao walishindwa kumudu gharama za dawa, huku wengine wakilazimika kununua kwa bei ya juu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na wadau wa Sekta ya Afya pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kufungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Dunia la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (WFNS) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam Aprili 16, 2026.
Alisema kilichomgusa zaidi ni mateso ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma au dawa kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yao. Hivyo alijiapiza kuboresha taasisi hiyo ili iwe kituo cha kisasa kinachoweza kutoa huduma bora si tu kwa Watanzania bali pia kwa ukanda mzima.