Matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yafikia asilimia 23.4  

Arusha. Serikali imeendelea kuimaisha jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia huku matumizi ya huduma hiyo yakiongezeka hadi kufikia asilimia 23.4 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021.

Hata hivyo, tayari Serikali imeweka mkakati wa kitaifa kuhakikisha hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ili kulinda afya na mazingira.

Akizungumza katika mjadala wa wadau uliojadili njia bora za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, leo Aprili 17, 2026 jijini Arusha, mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Emilian Nyanda, amesema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa mkakati maalumu ulioanza Mei 2024.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa nishati safi ya kupikia na kuweka malengo mahsusi ya kuongeza upatikanaji wake nchini, ambapo wakati mkakati unaandaliwa kiwango cha matumizi kilikuwa chini ya asilimia 10.

Kwa mujibu wa Nyanda, moja ya mbinu muhimu iliyochangia mafanikio hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu faida za kutumia nishati safi pamoja na madhara ya kutumia nishati chafu kama kuni na mkaa.

“Kwa sasa kiwango kimeongezeka sasa tumefikia asilimia 23.4 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia, hii inaonyesha kwamba kupitia mkakati huu wa kitaifa umeanza kutusaidia na moja ya mbinu tunaoztumia ni kujenga uelewa kwa jamii kuhusu mkakati, umuhimu wa kutumia nishati safi na changamoto za kutumia nishari zisizo safi,” amesema.

Nyanda amesema mkakati huo unatoa mwongozo wa namna ya kufikia lengo lililowekwa na Serikali ambapo kuna maboresho ya kisera na ushiriki wa wadau mbalimbali.

Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ni mdau muhimu katika utekelezaji wa mkakati huo, kutokana na ukweli kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wanategemea rasilimali za misitu kama chanzo kikuu cha nishati.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Joseph Makero ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotony kilichopo Arusha, amesema juhudi zinafanyika kuhakikisha matumizi ya nishati safi yanaongezeka sambamba na uhifadhi wa misitu.

Ameeleza kuwa wizara imejikita katika maeneo makuu matatu ikiwemo kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza ukataji wa miti, kuendeleza matumizi ya mabaki ya viwanda vya misitu kama chanzo cha nishati, na kukuza teknolojia rahisi zitakazosaidia wananchi kutumia.

“Tunajua nishati zingine bado ni gharama kubwa lakini kupitia majadiliano mambo tuliyosisitiza ni kuhakikisha tunakuwa na sera rafiki ambazo zinaendana ili kuhakikisha wananchi wanapata suluhu ya kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi, hususan wanaoishi vijijini ambako ndiko kuna matumizi makubwa ya kuni na mkaa katika mipango yote ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), nchini Tanzania, Charles Tulahi amesema mjadala huo ni  sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia (Cook Fund) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU).

Amesema hapa nchini Fao imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hususan katika sekta ya kilimo.

Tulahi amesema Fao imekuwa ikihamasisha matumizi ya biogesi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kigoma, ambapo wafugaji wanahimizwa kutumia kinyesi cha mifugo kuzalisha gesi kwa matumizi ya nyumbani.

“Katika maeneo kama Karatu, tumehamasisha matumizi ya biogesi mashuleni na kwa watu binafsi. Lengo ni kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuboresha afya za wananchi na kupunguza ukataji wa miti,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi hizo pia zinawalenga makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wanafunzi, vijana na akina mama ili kuhakikisha uelewa wa matumizi ya nishati safi unaenea kwa vizazi vyote.

Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi kutoka  Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Duniani (WWF), Savinus Kessy amesema taasisi hiyo inashirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wizara ya Nishati, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Ofisi ya Rais, Tamisemi ili kuimarisha utekelezaji wa mkakati huo.

“Sisi tunajikita zaidi katika kujenga uwezo wa taasisi za Serikali pamoja na kushirikiana na sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuhakikisha mnyororo mzima wa thamani wa nishati safi unafanya kazi kwa ufanisi,” amesema

Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, wadau wanaendelea kutathmini sera zilizopo ili kubaini maeneo yenye changamoto na kuyafanyia maboresho kwa lengo la kuhakikisha usimamizi bora na mafanikio ya muda mrefu.