Kijuso aanika mikakati mipya Bigman FC

KOCHA Mkuu wa Bigman FC, Mohamed Kijuso amesema kutimiza malengo ya awali ya timu hiyo ya kumaliza nafasi nne za juu ni ngumu kwao kutokana na ushindani uliopo, ingawa kwa sasa wataendelea kupambana ili kubakia kwenye ligi msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kijuso amesema hadi sasa hawako sehemu mbaya kutokana na pointi walizonazo, japo jitihada na umakini zinahitajika hasa kwa mechi za ugenini ambazo ugumu wake huongezeka mara mbili zaidi ya nyumbani.

“Malengo yetu ya mwanzo yalikuwa ni kumaliza nafasi nne za juu na kucheza mechi za ‘Play-Off’, japo kwa hali ilivyo ni ngumu kutimiza hilo, tunachopambana kwa sasa ni kutengeneza mazingira mazuri ya kubakia Championship,” amesema Kijuso.

Kocha huyo wa zamani wa Cosmopolitan, amesema licha ya timu hiyo kutokuwa na balansi nzuri katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji, kwa sasa anachozingatia ni kikosi hicho kinapata matokeo mazuri, bila ya kujali aina ya uchezaji.

Bigman FC iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Mwadui, katika mechi 22 ilizocheza msimu huu, imeshinda saba, sare sita na kupoteza tisa, ikifunga mabao 19 na kuruhusu 21 na iko nafasi ya nane na pointi 27.