UONGOZI wa timu ya Malindi, umethibitisha kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali ambapo nafasi yake imechukuliwa na Ally Ramadhani Kisaka, ikiwa ni miongoni mwa mikakati ya kupambana kuibakisha timu Ligi Kuu Zanzibar.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Malindi, Ramadhan Sanga wakati akizungumza na Mwanaspoti kisiwani hapa.
“Ni kweli Malindi imeachana na Kocha Hababuu na sasa benchi la ufundi linaongozwa na Kisaka, tumefanya hivyo kwasababu aliyemleta kwasasa ameshaondoka na hatujui makubaliano yalikuwaje,” amesema.
Alieleza kuwa, Kocha Hababuu hakuwa amefanya mazungumzo na uongozi uliopo sasa ndiyo maana baada ya mabadiliko kufanyika wakaamua kutafuta mwingine kuziba nafasi hiyo.
Meneja Sanga amesema kazi ya kocha huyo mpya itaonekana rasmi kwenye mechi dhidi ya KMKM itakayochezwa Mei Mosi mwaka huu kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.
Awali, kocha Hababuu alizungumza na Mwanaspoti baada ya kutoonekana kwenye mechi kati ya Malindi na JKU iliyomalizika kwa timu hiyo kufungwa mabao 4-1.
Kocha huyo, amesema hakufika uwanjani kwasababu timu hiyo haikumtafuta kwa ajili ya mazungumzo, hivyo asingejua anatoa wapi maslahi yake kwani aliyemleta ameondoka.
“Mimi hoja yangu nilitaka wanitafute tuzungumze nijue masilahi yangu lakini hawajanitafuta, hivyo mimi sijaachana nao ila wao wameachana na mimi,” amesema Hababuu.
Malindi kwasasa inapambana kujinasua na mtego wa kushuka daraja kwani inashika nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar baada ya kucheza mechi 22 ikikusanya pointi 24, imebakiwa na mechi nane kumaliza msimu.
