KIUNGO mshambuliaji wa Mbuni FC ya jijini Arusha, Joseph Mkele ‘Jojo’ amesema licha ya ushindani uliopo katika Ligi ya Championship ila mwenendo wake ni mzuri tangu alipojiunga na timu hiyo msimu huu akitokea KVZ FC ya visiwani Zanzibar.
Nyota huyo aliyewika pia na Mtibwa Sugar, amesema msimu uliopita ulikuwa mgumu kwake kutokana na ugeni wake wa Ligi Kuu ya Zanzibar, ingawa tangu amejiunga na Mbuni FC inayoshiriki Ligi ya Championship, kuna mabadiliko makubwa yanaonekana.
“Yaliyotokea msimu uliopita yalikuwa ni kipimo kizuri kwangu cha kunifundisha na kunikuza pia kiakili, ilikuwa ni wakati mgumu sana, ila nashukuru nilichukulia kama changamoto na kwa kiasi fulani naona matunda yake taratibu,” amesema Mkele.
Kiungo huyo aliyeifungia Mbuni mabao manne ya katika ligi hiyo hadi sasa, amesema licha ya timu hiyo kushika nafasi ya sita na pointi 38, ila wataendelea kupambana ili kumaliza ndani ya nne bora na kucheza mechi za ‘Play-Off’.
Nyota huyo anakumbukwa msimu wa 2020-2021 akiwa na timu ya vijana ya Mtibwa Sugar chini ya miaka 20, iliyotwaa ubingwa na aliibuka na tuzo mbili na kikosi hicho kutokea Morogoro ambazo ni ya kiungo bora na mchezaji bora wa mashindano.
