Serikali yafichua kilio cha vijana Tanzania

Dar es Salaam. Uhaba wa ajira, masilahi duni katika vibarua, ugumu wa miundombinu ya biashara na hofu ya kutoa maoni, ni baadhi ya changamoto kubwa zinazotajwa kumkabili kijana wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, changamoto hizo, zimeibuliwa katika hoja 186 zilizotolewa na vijana kutoka mikoa sita ambayo ni Songwe, Mbeya, Ruvuma, Mtwara, Dar es Salaam na Dodoma.

Katika changamoto zote hizo zilizotajwa na vijana kwa waziri wa wizara hiyo, Joel Nanauka alipowatembelea mikoani humo, ajira ndicho kilichokuwa kilio kikuu, kikifuatiwa na masilahi duni katika vibarua, kisha miundombinu duni ya kibiashara.

Hata hivyo, Serikali imesema itaendelea kupokea maoni na mapendekezo ya vijana na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo. Pia, itakuza majadiliano ya kitaifa kupitia kongamano la wajasiriamali na bodaboda.

Hayo yameelezwa leo, Jumatatu Aprili 20, 2026 na Nanauka, wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27, aliyoitoa bungeni jijini Dodoma ya Sh35.95 bilioni.

Katika hotuba hiyo, Nanauka amerejea ziara alizozifanya katika mikoa hiyo sita, akisema alitembelea maeneo 18 ambayo vijana wanafanyia kazi na kuwafikia jumla ya vijana 8,120.

Ziara hiyo, amesema iliibua hoja 186 zilizotolewa na kundi hilo, huku ukosefu wa ajira ikiongoza kwa kutolewa kwa asilimia 13.47 kati ya hoja zote zilizoibuliwa.

Hoja nyingine zilizotolewa zaidi kwa mujibu wa Nanauka, ni masilahi duni ya vibarua wanavyofanya kwa asilimia 9.68, miundombinu ya kufanyia biashara kutokuwa rafiki asilimia 9.68 na changamoto za usafiri na usafirishaji asilimia 9.82.

Kwa upande wa hoja ya upatikanaji wa mikopo ya asilimia nne kwa mapato ya ndani ya halmashauri, imeibuliwa kwa asilimia 10.52, kisha ukosefu wa mitaji ikiibuliwa kwa 10.53 na vigezo vigumu vya mikopo ya elimu ya juu asilimia 6.99.

Nanauka amesema hoja nyingine iliyoibuliwa ni hofu ya kutoa maoni kwa asilimia 6.45, mfumo wa elimu usioendana na soko la ajira asilimia 5.91, utitiri wa kodi na ushuru asilimia 5.03 na kutokuwa na elimu ya ujasiriamali asilimia 4.84.

Suala la urasimu wa kupata leseni na vibali, ni hoja nyingine iliyoibuliwa na vijana katika ziara hizo kwa asilimia 4.23, huku kukosekana kwa Baraza la Vijana la Taifa ikiibuliwa kwa asilimia 3.23.

“Takwimu hizo zinaonesha kuwepo kwa uelewa na mwamko wa vijana katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisera. Aidha, zoezi hili limekuwa chachu ya uwajibikaji, ushiriki wa vijana katika maendeleo na kujiamini katika kutoa maoni,” amesema.

Amesema hayo yote yameshuhudiwa baada ya kuundwa kwa wizara hiyo na kuwepo kwa dhamira ya kufahamu kwa kina mahitaji ya vijana, mawazo na mitazamo yao kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maisha yao ya kila siku.

“Wizara iliandaa ziara za kukutana na vijana kwa lengo la kutoa jukwaa la wazi la kusikiliza sauti zao, kuelewa changamoto wanazokumbana nazo na kupokea mapendekezo yao. Jitihada hizo zimewezesha Ofisi ya Rais-Maendeleo ya Vijana kuelewa changamoto za vijana,” amesema katika hotuba hiyo.

Amesema hiyo inatoa nafasi ya kuandaa na kutekeleza mipango na mikakati inayolenga kuboresha elimu ya uraia, kukuza uzalendo na kuwajengea vijana mazingira bora ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Amesisitiza wizara hiyo itaendelea kupokea maoni na mapendekezo na changamoto za vijana na kuzitafutia ufumbuzi.