Kiungo wa Young Africans SC, Mudathir Yahya, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni moja kufuatia kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji FC, Ibrahim Abraham, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Adhabu hiyo ni sehemu ya maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu ya NBC (TPLB) katika kikao chake cha Aprili 18, 2026, ambapo ilipitia matukio mbalimbali ya kinidhamu yaliyojitokeza katika michezo tofauti ya ligi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, Mudathir alipatikana na hatia chini ya Kanuni ya 41:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji, kufuatia tukio hilo lililotokea wakati mchezo ukiendelea. Kufungiwa kwake kunamaanisha kuwa Young Africans SC italazimika kumkosa kiungo huyo muhimu katika michezo mitatu ijayo ukiwemo ule wa dabi ya Kariakoo utakaopigwa Mei 3, hali inayoweza kuathiri mipango ya kiufundi ya timu hiyo katika kipindi hiki muhimu cha msimu.
Mbali na adhabu hiyo, TPLB pia imechukua hatua kali dhidi ya klabu mbalimbali kufuatia matukio ya utovu wa nidhamu. Katika mchezo namba 07 uliochezwa Arusha, klabu za TRA United FC na Simba SC zimetozwa faini ya Sh5 milioni kila moja baada ya walinzi wao kupigana mara tu baada ya timu hizo kuwasili uwanjani.
Katika mchezo mwingine uliopigwa Tanga, Coastal Union FC ilitozwa faini ya Sh5 milioni kutokana na mashabiki wake kurusha chupa za maji uwanjani wakati wa vurugu zilizotokea kufuatia mchezaji wa Mtibwa Sugar FC, Victor Collins, kumsukuma Athuman Makambo wa Coastal Union.
Aidha, Singida BS nayo imejikuta ikiadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh5 milioni baada ya viongozi wake wawili kuingia uwanjani na kumwaga vimiminika kabla ya mchezo dhidi ya TRA United, kitendo kilichotafsiriwa kama ishara ya imani za kishirikina.
Katika mchezo kati ya Azam FC na Simba SC uliomalizika kwa suluhu, Azam metozwa faini ya Sh5 milioni kutokana na benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji kutumia mlango usio rasmi kuingia uwanjani kinyume na kanuni za mchezo.
Kwa upande wa Simba SC, klabu hiyo imepigwa faini ya Sh10 milioni baada ya mashabiki wake kumrushia chupa mwamuzi msaidizi, ikiwa ni kosa la kujirudia ndani ya msimu huu wa 2025/2026.
TPLB imesisitiza kuwa adhabu hizo zinalenga kuhakikisha nidhamu inazingatiwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikitoa onyo kwa klabu, wachezaji na mashabiki kuzingatia kanuni ili kulinda taswira ya soka la Tanzania.