Tanzania yapata bingwa wa kwanza wa magonjwa ya mfumo wa chakula kwa watoto

Dar es Salaam. Daktari Livin Mumburi ameandika historia mpya nchini baada ya kuwa daktari bingwa wa kwanza wa magonjwa ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kwa watoto, katikati ya changamoto ya magonjwa ya mfumo wa chakula kwa watoto.

Kwa mujibu wa ukurasa wa mtandao wa kijamii wa African Pediatric Fellowship wa Facebook, Dk Mumburi ameandika historia hiyo baada ya kuhitimu kwa mafanikio makubwa ubingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula kwa watoto kupitia Chuo cha Tiba cha Afrika Kusini, hatua inayomuweka miongoni mwa wataalamu wachache barani Afrika katika fani hiyo.

Akiwa anatarajia kurejea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), uwepo wake unatarajiwa kuleta mapinduzi katika huduma za afya kwa watoto.

Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu, Aprili 20, 2026, kuhusu umuhimu wa utaalamu huo, Dk Mumburi amesema mahitaji ya huduma za kibingwa kwa watoto wenye matatizo ya mfumo wa chakula na ini ni makubwa kuliko ilivyodhaniwa.

“Uhitaji ni mkubwa sana, kwa sababu hata kabla sijaenda kufanya mafunzo ya ubingwa nilikuwa nakutana na watoto wengi wenye changamoto kubwa za mfumo wa chakula na magonjwa ya ini. Hii inaonesha wazi bado tuna pengo kubwa la wataalamu katika eneo hili,” amesema.

Ameongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika ili kuongeza idadi ya wataalamu wa fani hiyo nchini.

“Bado tunahitaji wataalamu wengi zaidi. Naangalia namna gani naweza kuwahamasisha na kuwaongoza wengine waingie katika eneo hili ili tupanue huduma na kuwafikia watoto wengi zaidi wanaohitaji matibabu haya maalum,” amesema Dk Mumburi.

Mumburi ni daktari aliyebobea katika utambuzi na matibabu ya matatizo ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kwa watoto wachanga hadi balehe, baada ya kupitia mafunzo ya udaktari wa watoto na kuongeza utaalamu maalum wa magonjwa ya njia ya chakula (GIT).

Watoto wengi nchini hukumbwa na changamoto za muda mrefu kama utapiamlo, matatizo ya ini, vidonda vya tumbo, na magonjwa sugu ya utumbo ambayo mara nyingi hukosa utambuzi wa kina.

Kwa mujibu wa mtandao huo, upatikanaji wa mtaalamu huyu utasaidia kupunguza rufaa za nje ya nchi, gharama kubwa za matibabu, na vifo vinavyoweza kuzuilika.

Mbali na taaluma yake, Dk Mumburi anasifiwa kwa unyenyekevu, huruma na ucheshi wake, sifa zinazomfanya kuwa tegemeo si tu kwa wagonjwa wadogo bali pia kwa wazazi wao. Uwepo wake ni hatua muhimu katika kuimarisha ubora wa huduma za kibingwa nchini.