Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema itaendelea kutumia afua mbalimbali za kukabiliana na malaria ikiwamo teknolojia mpya ya kubadili vinasaba vya mbu wanaoeneza ugonjwa huo, ili kutokuwa na uwezo wa kuueneza (Gen drive).
Hafua zingine ambazo Serikali imesema zitatumika pamoja kukabiliana na ugonjwa huo ni matumizi ya vyandarua pamoja na viatilifu vya kuua mazalia ya mbu.
Kauli hiyo, imetolewa Aprili 17, 2026 mjini Bagamoyo na Mkurugenzi wa Sera, Tafiti na Ubunifu kutoka Wizara ya Afya, Dk Tumainiel Macha wakati akielezea mipango ya wizara hiyo katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria katika mkutano wa wataalamu mbalimbali ulioratibiwa na Muungano wa Viongozi wa Kupambana Malaria Afrika (ALMA).
Utafiti wa ubadilishaji wa vinasaba kwa mbu waenezao malaria ili kuwaondolea sifa ya kusababisha ugonjwa huo, unatekelezwa na Taasisi ya Afya Ifakara (IHI) Bagamoyo.
Dk Macha amesema ugonjwa wa malaria bado ni tishio nchini na katika kukabiliana nayo, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuutokomeza ili jamii iishi bila ugonjwa huo.
“Ukiangalia tafiti nyingi duniani pamoja na afua mbalimbali zinazotumika kudhibiti malaria, dunia inaelekea kwenye afua hii ya ubadilishaji wa vinasaba ambayo tunaifanyia utafiti ili tuanze kuitumia,” amesema.
Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti Ifakara (ihi), Fatuma Matwewe akielezea namna wanavyobadili vinasaba vya mbu ili wakose uwezo wa kueneza malaria.
Amesema tayari jamii imeendelea kushirikishwa kwenye utafiti huo ili uje kuwa na matokeo chanya na ifikapo 2030 mbu hao wanaotengenezwa wataachiwa kwenye jamii rasmi ili kuanza kuona matokeo yao.
Kauli hiyo ya Serikali inakuja ikiwa ni hatua za kuanza kwa kampeni ya elimu juu ya malaria itakayohitimishwa Aprili 25 ni Siku ya Malaria Duniani.
Katika kuelekea maadhimisho hayo, Wizara ya Afya imetaja makundi yanayoathirika zaidi na malaria kuwa ni wajawazito, watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea na watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU).
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika mapambano ya malaria, Mkurugenzi Mwandamizi wa ALMA, Dk Abraham Mzava amesema wanatambua Tanzania inaushawishi mkubwa wa kutoa uongozi katika kukabiliana na ugonjwa huo.
Amesema mchango wao kwa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika, ni namna taasisi hiyo inavyosaidia uratibu wa fedha zaidi ya Sh200 bilioni kwa ajili ya kupambana na mbu waenezao malaria.
Dk Mzava amesema taasisi hiyo haifanyi tafiti bali wanategemea taasisi zingine kufanya tafiti zenye kujibu changamoto za wananchi ikiwamo, uwepo utafiti wa kubadili vinasaba vya mbu waenezao malaria, utafiti alioutaja kuendeleza juhudi za kukomesha malaria.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Ifakara (IHI), Dk Honorati Masanja amesema utafiti wa ubadilishaji wa mbu, vinasaba wanaufanya kwa kuzingatia sifa za kitaifa na kimataifa kwenye jamii.
Amesema utafiti huo ukianza kutumika utakuwa na matokeo chanya kwenye jamii ambayo sasa maambukizi ya malaria yanaendelea huku baadhi ya maeneo maambukizi ni asilimia moja, tano na nane kwa baadhi ya maeneo.
“Yapo maeneo ambayo maambukizi ya malaria ni makubwa ikiwamo Kanda ya Ziwa lakini maeneo mengine maambukizi yapo chini ikiwamo Mkoa wa Arusha na Dodoma, kwa hiyo juhudi hizi za teknolojia zitasaidia kukabiliana na malaria,” amesema.
Teknolojia ya ubadilishaji wa mbu kwa kutumia vinasaba inaibuka kama suluhisho jipya katika mapambano dhidi ya malaria, ugonjwa unaoendelea kuathiri mamilioni ya watu barani Afrika.
Kupitia mbinu za kisasa kama CRISPR-Cas9, wanasayansi hubadilisha jeni za mbu, hasa Anopheles gambiae ili kupunguza uwezo wao wa kueneza maambukizi.
Mbinu ya “gene drive” huruhusu jeni hizi kuenea haraka katika vizazi, hivyo kupunguza idadi ya mbu wanaoweza kubeba vimelea.
Watafiti pia huchunguza uwezekano wa kuachilia mbu waliobadilishwa ambao hawawezi kuzaa au kusambaza malaria.
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyoitwa Plasmodium ambavyo husambazwa kutoka kwa mtu mmoja, kwenda kwa mwingine kwa kung’atwa na mbu jike aina ya ‘Anopheles’ mwenye vimelea.
Mikoa kadhaa, ikiwamo Songwe, Njombe, Arusha, Manyara na Kilimanjaro ina kiwango cha maambukizi ya malaria kilicho chini ya asilimia moja, wakati mikoa ya kusini na kaskazini-magharibi mwa nchi ikiwa na kiwango cha maambukizi ya malaria kilicho juu ya asilimia 20.
Takwimu za utafiti wa viashiria vya malaria katika jamii wa mwaka 2022, kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kimepungua kwa asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Kwa mujibu kwa takwimu za Wizara ya Afya, idadi ya vifo vitokanavyo na malaria imepungua kwa asilimia 39 kutoka vifo 2,460 mwaka 2020 hadi kufikia vifo 1,503 mwaka 2024.
Mikoa mitano inayoongoza kwa maambukizi ni Tabora kwa asilimia 23.4, Mtwara asilimia 19.7, Kagera (17.5) Shinyanga (15.6) na Mara (15.1).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 15 ya watu kutoka kaya maskini huathiriwa na malaria ikilinganishwa na asilimia moja kwa kaya tajiri.
