*************
Na Sixmund Begashe, Njombe
Club ya Michezo ya Wizara ya Maliasili na Utalii leo tarehe 20 Aprili ,2026 imeungana na Club zingine za Wizara na Taasisi mbalimbali pamoja na wakazi wa Njombe, kwenye ufunguzi rasmi wa Michezo ya Mei Mosi 2026 Mkoani Njombe.
Akizindua Michezo hiyo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Rahma Kisuo, ametoa wito kwa taasisi zote za umma na binafsi nchini kutambua umuhimu wa michezo na kuhakikisha wafanyakazi wanashiriki kikamilifu.
Mhe. Kusuo amesema michezo ni msingi wa afya bora, akibainisha kuwa afya ya mfanyakazi ni mtaji mkubwa unaochochea maendeleo ya taasisi na Taifa kwa ujumla hivyo ushiriki wao katika michezo ni jambo la msingi.
Aidha, amewahimiza wafanyakazi kote nchini kuendeleza utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara, akisisitiza kuwa mazoezi yasifanywe wakati wa mashindano pekee bali yawe sehemu ya maisha ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Kisuo amewapongeza washiriki wote wa michezo hiyo na kuwaasa kuzingatia nidhamu, mshikamano pamoja na ushindani wa haki.
Kwa mwaka 2026, Michezo ya Mei Mosi inaongozwa na kauli mbiu isemayo:
*“Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”*



