Simiyu. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wachimbaji wadogo mkoani Simiyu kuacha kutumia mifumo isiyo rasmi ya kifedha na badala yake kujikita katika matumizi ya huduma rasmi za benki na taasisi za fedha ili kuongeza usalama wa mapato yao na kuchochea maendeleo ya sekta ya madini.
Akizungumza Aprili 21, 2026 wakati wa mafunzo ya ujuzi wa kifedha kwa wachimbaji, Mwakilishi wa BoT, Mipawa Yesse amesema kuwa matumizi ya mifumo rasmi ya fedha yatasaidia kupunguza hatari ya upotevu wa fedha, kuimarisha uwazi katika miamala na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha.
Amesema wachimbaji wengi bado wanatumia njia zisizo rasmi kuhifadhi au kuhamisha fedha, hali inayowafanya kushindwa kujenga historia ya kifedha inayoweza kuwasaidia kupata mikopo au huduma nyingine muhimu za kifedha.
Sehemu ya watumishi wa BOT walioshiriki kutoa mafunzo ya ujuzi wa kifedha kwa wachimbaji wadogo wa mkoa wa mkoa wa Simiyu.Picha na Samwel Mwanga
“Tunawahimiza wachimbaji kufungua akaunti benki, kutumia huduma za fedha na kushirikiana na taasisi zilizosajiliwa ili kulinda mapato yao na kukuza shughuli zao,” amesema.
Amesema kuwa BoT inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo benki za biashara na watoa huduma za fedha kwa njia ya simu ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wengi zaidi, hususan walioko maeneo ya vijijini.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo mchimbaji mdogo Jonas Marwa amesema kuwa bado wanakumbana na changamoto za uelewa mdogo wa huduma za kifedha pamoja na umbali wa kufikia matawi ya benki, hali inayowalazimu kuendelea kutumia njia zisizo rasmi.
“Mie nikiri kabisa sisi wachimbaji wadogo tulio wengi bado hatuna uelewa wa huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi mbalimbali za fedha kama vile benki ila tunahitaji mafunzo kama haya mara kwa mara,” amesema.
Naye Juliana Mgaya ambaye pia ni mchimbaji mdogo wilaya ya Bariadi ameipongeza BoT kwa juhudi za kutoa elimu ya fedha.
“Hatua hii ya BoT kutupatia mafunzo itasaidia kuongeza uelewa na kuwahamasisha wachimbaji wengi kuingia katika mfumo rasmi,’amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ujuzi wa kifedha kwa wachimbaji wadogo wa mkoa huo, mafunzo ambayo yanatolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Picha na Samwel Mwanga
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Anamringi Macha amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuhakikisha sekta ya madini inachangia ipasavyo katika uchumi wa taifa.
“Sekta ya madini ina mchango mkupwa katika uchumi wa taifa letu kwa mkoa wa Simiyu tu sekta hiyo imechangia kiasi cha Sh4.3 bilioni kwa mwaka wa fedha uliopita na ni wachimbaji wadogo,hivyo mafunzo haya yanayotolewa na BoT ni muhimu sana,” amesema.

