Morogoro. Watu watatu wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha basi la abiria na lori, tukio lililotokea eneo la Kona S’, Kata ya Kidodi, Mikumi wilayani Kilosa, mkoani Morogoro.
Ajali hiyo imetokea asubuhi ya Aprili 21, 2026 ambapo basi la abiria la kampuni ya ZL Supper lililokuwa likitoka Ifakara kuelekea Dodoma, likiendeshwa na Emanuel Benito, liligongana uso kwa uso na lori lililokuwa likitokea Mikumi kwenda Ruaha, likiendeshwa na Yasin Nasir.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, amesema chanzo cha ajali hiyo kinadaiwa kuwa ni uzembe wa dereva wa lori aliyekuwa akijaribu kuipita pikipiki ya magurudumu matatu (Toyo) bila kuchukua tahadhari.
Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Kilosa wakifanya uokozi kwenye ajali iliyohusisha basi la abiria la kampuni ya ZL ambalo limegongana uso Kwa uso na lori la mizigo eneo la kosa S barabara ya Mikumi – Ruaha wilaya ya Kilosa. Picha Hamida Shariff
Amesema waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni dereva wa lori, Yasin Nasir (48), pamoja na abiria wawili wa basi hilo, Awadh Ngwanda (60) na Zalaph Awadh (20).
Kwa mujibu wa Kamanda Kantimbo, majeruhi watano katika ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi kwa matibabu, ambapo hali zao zinaendelea kuimarika.
Kufuatia tukio hilo, amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Askari wa jeshi la zimamoto na uokoaji Wilaya ya Kilosa akikagua magari mara baada ya kufanya ukaguzi kwenye ajali iliyotokea eneo la kosa S barabara ya Mikumi – Ruaha wilaya ya Kilosa, katika ajali hiyo watu watatu wamefariki dunia na wengine watano wajeruhiwa. Picha Hamida Shariff
Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro, Shabani Marugujo amesema kikosi chake kilifika eneo la tukio kwa haraka na kuanza operesheni ya uokoaji kwa kutumia vifaa maalumu.
Ameeleza kuwa walitumia mashine za kukatia vyuma (Hydraulic Cutter) na kupanua (Expander) ili kuwaokoa majeruhi waliokuwa wamenaswa kwenye vyombo hivyo pamoja na kutoa miili ya marehemu.
Amesema kati ya miili mitatu iliyotolewa, mmoja alikuwa dereva wa lori huku miwili ikiwa ya abiria waliokuwa ndani ya basi hilo.
