Mapinduzi ya akili unde yashika kasi elimu ya juu

Dar es Salaam. Katika hatua ya kuimarisha ubora wa huduma na kuongeza tija ya taasisi, wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wametakiwa kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI), wakionywa kuwa kushindwa kuendana na kasi ya mageuzi ya kidijitali kunaweza kudhoofisha ufanisi wa taasisi.

Rai hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Moremi Marwa, wakati akifungua Mkutano Maalumu wa Baraza la Wafanyakazi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza, akisisitiza kuwa teknolojia si chaguo tena bali ni nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji wa kila siku.

“Katika zama hizi za mabadiliko ya haraka, teknolojia hususan akili unde ina nafasi kubwa katika kurahisisha kazi, kuboresha huduma na kusaidia kufanya maamuzi sahihi ya kitaasisi,” amesema Marwa.

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi wa chuo hicho uliofanyika leo Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam

Marwa ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ameongeza kuwa pamoja na matumizi ya teknolojia, wafanyakazi wanapaswa kuendelea kuzingatia misingi ya uadilifu na uwajibikaji ili kuimarisha imani ya jamii na wadau wa elimu ya juu.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye, amesema taasisi hiyo inaendelea kupiga hatua kubwa za kimkakati chini ya Dira ya Chuo ya mwaka 2061 na Mpango Mkakati wa miaka 10 (2024–2033), hatua inayolenga kulifanya chuo kuwa kitovu cha ubora wa elimu na utafiti.

Amebainisha mafanikio yaliyopatikana katika maeneo manne muhimu, yakiwemo kuimarika kwa mifumo ya ndani, nidhamu ya fedha, ustawi wa watumishi na kuongezeka kwa utambuzi wa mchango wa wafanyakazi.

Katika eneo la usimamizi wa fedha, Profesa Anangisye amesema chuo kimefanikiwa kupata hati safi za ukaguzi kwa miaka minne mfululizo, huku hoja za ukaguzi zikishuka kutoka 86 hadi 34, ishara ya kuimarika kwa uwajibikaji wa kifedha.

Kuhusu ustawi wa watumishi, amesema chuo kimetumia Sh1.15 bilioni kununua viwanja 161 kwa ajili ya wafanyakazi kujenga makazi, sambamba na kuanza kutekeleza mpango wa motisha ulioidhinishwa mwaka 2024.

Baadhi ya wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) walioshiriki katika Mkutano Maalum wa Baraza la Wafanyakazi wa chuo hicho uliofanyika leo Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam

Hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na ununuzi wa basi la wafanyakazi ili kurahisisha usafiri na maboresho ya utaratibu wa upandishaji vyeo kwa wanataaluma, ambapo sasa utafanyika kila robo mwaka badala ya mara moja kwa mwaka.

Aidha, chuo kinaendelea kunufaika na mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa Uchumi (HEET), unaochangia kuboresha miundombinu ya kufundishia, utafiti na kuharakisha mageuzi ya elimu ya kidijitali.

Mkutano huo umetajwa kuwa jukwaa muhimu la kupokea maoni ya wafanyakazi, kutathmini utendaji na kuweka mikakati ya kuendelea kuboresha huduma za chuo hicho, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuchangia kwa ufanisi maendeleo ya taifa kupitia elimu bora na ubunifu.