Dar es Salaam. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhasham Askofu Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Lindi, amesema marehemu Askofu Bernardin Mfumbusa hakuwa mtu wa kukaa kimya mbele ya uovu.
Askofu Mfumbusa alifariki dunia Aprili 14, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma.
Akizungumza katika misa takatifu ya mazishi ya Askofu Mfumbusa iliyofanyika leo Aprili 22, 2026 katika Jimbo Katoliki Kondoa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wastaafu, Askofu Pisa amesema marehemu hakuwa tayari kuvumilia mambo yasiyoenda sawa, hususan yanayohusiana na uovu.
Akizungumzia ukweli na uwazi kuhusu maisha ya Askofu Mfumbusa, amesema hakuwa muumini wa kufumbia macho uovu, huku akieleza kuwa, kukalia kimya uovu pia ni uovu.
Mwili wa aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Askofu Bernadin Mfumbusa ukiingizwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Amesema, hakuwa mtu wa kukaa kimya bali lazima azumgumze.
“Kuna mwanateorojia maarufu kutoka Ujerumani alinyongwa Aprili, 1945 aliyekuwa anaitwa Dietrich Bonhoeffer, yeye alisema ukimya katika uovu ni uovu maana yake hakuna njia ya katikati ni aidha unakubali au unaikataa dhambi.
“Baba Mfumbusa alikuwa wa namna hiyo, hakai kimya lazima azungumze na lazima akupigie simu au akufuate kukwambia. Hakuna njia ya katikati ni aidha unatenda au hutendi,” amesema.
Alisema Askofu Mfumbusa alitamani kuwatoa watu katika nyika la dhambi na alikuwa na lengo la kuwainua watu kitaaluma kama njia ya kuwatoa katika nyika.
Alisema katika utendaji wake, Askofu Mfumbusa aliisikiliza na kuitii sauti ya Mungu. Yote aliyafanya kama mapenzi ya Mungu katika maisha yake.
Kwa mujibu wa TEC, upande wa taaluma yake ya mawasiliano kiongozi huyo ameitendea haki na kukuza waandishi wengi nchini.
Imeeleza kuwa, Askofu Mfumbusa ametoa mchango mkubwa wa kuendeleza kitivo cha mawasiliano alipokuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino.
Askofu Agapiti Ndorobo amesema lipo deni kubwa la kuiga yale yote aliyofundisha na kuyafanya huku akitoa wito wa kuendelea kukumbuka mafundisho yake.
Makamu wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Dk Philip Mpango amesema kitendo cha Askofu Mfumbusa kufanya jitihada za kuinua uchumi wa kanisa kupitia kilimo, kinapaswa kuigwa ili watu watakapostaafu waboreshe maisha kupitia kilimo.
Amesema kanisa na Taifa kwa jumla, limepoteza kiongozi mahiri aliyejikita katika kilimo eneo la Zanka mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akitoa heshima za mwisho mara baada ya kushiriki ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, marehemu Askofu Bernadin Mfumbusa, iliyofanyika jana Aprili 21, 2026 Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatma Nyangasa amesema elimu ya kina ya dini na duniani aliyoipata Askofu Mfumbusa ni nafasi ya kipekee aliyoipata kisha kuitumia katika jamii yetu.
“Tumepata hekima na busara zake bila kusahau usikivu wa kila mmoja wetu. Ameacha alama ya upendo na mshikamano na tutaendelea kuziishi nguzo hizo muhimu alizotuachia,” amesema.
Alikuwa kiungo wa madhehebu mengine
Jana, Jumanne Aprili 21, 2026 Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Emmanuel Nchimbi alisema Taifa litaukumbuka mchango mkubwa alioutoa marehemu Askofu Mfumbusa, enzi za uhai wake ikiwamo kuwa kiungo muhimu wa kuunganisha Kanisa Katoliki na madhehebu mbalimbali pamoja na dini zingine.
Makamu wa Rais alisema hayo baada ya kushiriki ibada ya kumuaga na kumuombea Askofu Mfumbusa, iliyofanyika Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Alisema marehemu alijitolea kuunganisha dini na madhehebu ili zifanye kazi kwa kuheshimiana, kushirikiana na kupendana.
Dk Nchimbi alisema Taifa litakumbuka mchango wake katika kuhamasisha elimu pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha na kusimamia ujenzi pamoja na uendelezaji wa huduma za afya katika Wilaya ya Kondoa na Taifa kwa jumla.
Makamu wa Rais alisema Askofu Mfumbusa ametoa mchango katika sekta ya mawasiliano na habari akiwa mbobezi na mwalimu katika fani hiyo.
“Marehemu Mfumbusa atakumbukwa kwa kutimiza wajibu wake kwa binadamu kwa kutambua maisha tunayoishi leo na kutimiza wajibu wake kwa Mungu kwa kutuongoza katika njia ya uzima wa milele,” alisema.
Kufuatia kifo hicho, Papa Leo XIV ametuma salamu za rambirambi kupitia Balozi wa Papa (Vatican) nchini Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accatino huku akitoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki.
Askofu Accatino amesema Aprili 9, 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV alimteua Askofu Mfumbusa kuwa Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (CEPACS) na wakati huohuo alikuwa ameteuliwa siku chache kuwa mjumbe wa Bodi ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano.