KIUNGO mshambuliaji wa Fountain Gate, Mrundi Elie Mokono ameanza mazoezi na timu hiyo baada ya kukosekana katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopita waliposhinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar iliyopigwa Aprili 18, 2026.
Nyota huyo alipata majeraha katika mechi ya kichapo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba, Aprili 15, 2026, baada ya kugongana na mwenzake, Mrundi Derrick Mukombozi na kutoka dakika ya 19, kisha kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Fountain Gate, Nahumu Muganda, alisema mchezaji huyo kwa sasa anaendelea vizuri na tayari ameshaanza mazoezi na wenzake, jambo ambalo ni jema kwake mwenyewe na benchi la ufundi kwa ajili ya mechi zijazo.
“Baada ya uchunguzi wa kina hospitalini alionekana alishtuka tu na haikuwa jeraha la kutisha, mechi yetu na Mtibwa Sugar angeweza kucheza lakini tuliona ni vyema kumpa muda zaidi wa kupumzika na kuangalia pia mwenendo wake,” alisema Muganda.
Muganda, alisema wakati Ligi Kuu ikiwa mapumziko kupisha michuano ya Kombe la Muungano inayoendelea visiwani Zanzibar, mchezaji huyo ataendelea na programu mbalimbali za benchi la ufundi, huku akitarajiwa kuanza kucheza rasmi mechi zijazo.
“Niwatoe hofu mashabiki zetu kuhusu hali ya Mokono, anaendelea vizuri na moja kwa moja ameanza mazoezi na kundi la nyota wenzake, tunatarajia kumuona uwanjani Aprili 30, 2026 katika mechi yetu na Pamba Jiji tutakayokuwa nyumbani,” alisema.
Kiungo huyo aliyejiunga na Fountain Gate, Agosti 1, 2024 akitokea Bumamuru FC ya kwao Burundi msimu wake wa kwanza wa 2024-2025 alifanya vizuri katika Ligi Kuu Bara baada ya kumaliza kinara akiwa na kikosi hicho kwa kufunga mabao saba.
Msimu huu wa 2025-2026, nyota huyo ameanza kwa kusuasua kutokana na majeraha mbalimbali, ambapo amechangia bao moja tu la Ligi Kuu lililofungwa na Sadick Ramadhan, katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City, Machi 3, 2026.