Washington. Benki ya Afrika ya Uagizaji na Usafirishaji Nje ya Nchi (Afreximbank) imesema iko tayari kuendelea kuisaidia Tanzania kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Aidha, benki hiyo imeeleza nia ya kuwekeza katika miradi mipya ya sekta ya madini pamoja na ujenzi wa hospitali kubwa ya kisasa itakayotoa huduma za matibabu kwa viwango vya kimataifa.
Ahadi hiyo imetolewa jijini Washington nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Afreximbank anayeshughulikia masuala ya biashara ya kimataifa, Haytham ElMaayergi.
Ametoa kauli hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, akizungumza kwenye kikao chao kilichofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, pembezoni mwa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF.
ElMaayergi amesema Tanzania ni mdau wa kimkakati wa benki hiyo na wako tayari kushirikiana nayo kutekeleza miradi mbalimbali itakayokubaliwa na pande zote mbili, yenye tija na itakayochochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania.
“Tuko tayari kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania katika mradi wa kununua na kuongeza thamani ya dhahabu, kuendelea kutafuta fedha za ujenzi wa reli ya SGR.
“Pia, tunasubiri kukamilika kwa mchakato wa kuwekeza katika kituo kikubwa cha matibabu ya kibingwa cha kiwango cha kimataifa nchini Tanzania,” amesema ElMaayergi.
Balozi Omar ameishukuru Afreximbank kwa kuendelea kuisaidia Tanzania, si tu katika kufadhili mradi wa reli ya kisasa ya SGR.
Ameipongeza kwa kusaidia shughuli za kibajeti za Serikali, ikiwamo nafasi yake kama mratibu mkuu wa upatikanaji wa fedha (Mandated Lead Arranger) katika muamala wa ufadhili wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Amesema wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa vipande vya sita na saba vya SGR kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inatarajia pia Afreximbank kushiriki katika mpango huo kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa uchumi wa nchi.
Balozi Omar ameiomba Afreximbank kufungua dirisha la ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuwawezesha waendelezaji wa miradi na makandarasi wakuu kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika sekta ya afya, alisema Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa Kituo cha Afrika cha Ubora wa Huduma za Tiba (AMCE), ambacho kinatarajiwa kuwa nguzo muhimu ya kuimarisha miundombinu ya afya nchini na katika ukanda mzima.
Kwa upande wa nishati ya mafuta, Balozi Omar ameipongeza Afreximbank kwa ushirikiano wake na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), pamoja na kuonesha nia ya kusaidia uagizaji wa bidhaa za petroli kwa kipindi cha Mei hadi Julai 2026.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa mpango huo katika kuhakikisha usalama wa nishati nchini.
