Moshi. Mama mzazi wa marehemu, Halima Mwakeraa, amesimulia namna binti yake, Asha Abdallah alivyomweleza kuhusu uamuzi wake wa kuvunja uhusiano wake na kijana anayedaiwa kumuua siku chache kabla ya tukio hilo kutokea.
Asha Abdallah, ofisa muuguzi katika Hospitali ya Mji Same, mkoani Kilimanjaro, aliyekuwa akifanya kazi ya kujitolea, aliuawa Aprili 20 mwaka huu katika makazi ya watumishi karibu na hospitali hiyo, muda mfupi baada ya kutoka kazini.
Akithibitisha tukio hilo jana, Aprili 21, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, alisema mauaji hayo yalitokea saa tatu usiku, baada ya mtuhumiwa kumfuata muuguzi huyo na kumchoma kisu shingoni.
“Mtumishi wa Hospitali ya Mji Same aliuawa kwa kuchomwa kisu na mpenzi wake anayedaiwa kumsaidia kimasomo. Tukio limetokea katika eneo la makazi aliyokuwa akiishi marehemu,” alisema Mgeni.
Aliongeza kuwa kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa alimpigia simu marehemu akimtaka wakutane, ndipo alipofika nyumbani kwake na kutekeleza mauaji hayo kisha kutoroka.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, marehemu alikuwa na uhusiano na wanaume wawili, huku mtuhumiwa akidaiwa kuwa ndiye aliyekuwa akimsaidia masomo yake hadi alipofikia hatua ya kupata ajira.
“Baada ya kuanza kazi, marehemu alidaiwa kuanzisha uhusiano mwingine na mtumishi mwenzake hospitalini hapo, jambo lililomkera mtuhumiwa na kusababisha tukio hili,” alieleza.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo na akipatikana atachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, Jumatano, Aprili 22, 2026, Halima amesema binti yake alimwomba wazungumze kuhusu jambo lililokuwa likimsumbua.
Amesema mtoto wake alikuwa muwazi kwake na hakumficha jambo lolote, hivyo alimweleza changamoto za kimahusiano aliyokuwa akipitia.
“Aliniambia, ‘Mama, kuna kitu nataka nikushirikishe, lakini nilikosea tangu mwanzo.’ Aliniambia alikuwa na rafiki waliyekubaliana kuoana, lakini wasubiriane hadi amalize chuo, alikuwa akimsaidia hata kumpa hela za matumizi,” ameeleza mama huyo.
Amesema binti yake alimweleza kuwa aliamua kuvunja uhusiano na kijana huyo baada ya kugundua kuwa na tabia zisizofaa, ikiwemo kuhusisha ndugu zake katika migogoro yao.
“Aliniambia hawezi kuendelea na uhusiano huo kwa sababu kila wakigombana, kijana huyo alikuwa anachukua uamuzi wa hatari. Kuna wakati alijaribu kujinyonga baada ya mwanangu kumwambia waachane,” amedai Halima.
Kwa mujibu wa mama huyo, hali hiyo ilimfanya binti yake achukue uamuzi wa kujitenga naye, lakini kijana huyo aliendelea kumfuatilia hadi siku ya tukio.
Kwa sauti ya uchungu, Halima ameeleza kifo cha binti yake ni pigo kubwa kwa familia yao, akieleza kuwa ndiye alikuwa tegemeo lao pekee.
“Alikuwa mtoto wangu wa mwisho na ndiye tuliyemtegemea kuikomboa familia. Ndugu zake walijitolea kumsomesha hadi kufikia hapa, wakati wengine waliishia kidato cha nne,” amesimulia kwa sauti ya mtetemo, huku akibubujikwa na machozi.
Hivyo, Halima ameiomba Serikali kuhakikisha mtuhumiwa anakamatwa na kufikishwa mahakamani ili haki itendeke.
Kwa upande wake, baba mzazi wa marehemu, Abdallah Bakari, amesema siku ya tukio binti yake alichelewa kurudi nyumbani, hali iliyomfanya aanze kumtafuta bila mafanikio.
“Nilimpigia simu mara kadhaa bila kupokelewa. Baadaye kijana mmoja alifika usiku na kuniambia binti yangu amepata tatizo, ndipo nikaenda naye eneo la tukio,” amesema.
Bakari amesema alipofika eneo la tukio, alikuta umati wa watu na mwili wa binti yake ukiwa chini katika makazi ya watumishi wa hospitali.
Bakari ameiomba Serikali, kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuingilia kati tukio hilo, akidai kuwa familia yake imewahi kupoteza ndugu mwingine katika mazingira ya mauaji bila haki kupatikana.
“Naomba msaada wa Serikali, tayari tumepoteza watu wawili katika mazingira kama haya bila haki kupatikana,” amesema.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Mbuyuni, Aminael Mghamba, amelaani kitendo hicho na kutoa wito kwa wananchi kuzingatia utatuzi wa migogoro kwa njia za amani badala ya kutumia vurugu.
Kuhusu maziko, Bakari amesema mwili wa binti yake umeshafanyiwa uchunguzi wa kitabibu, na familia inasubiri kukabidhiwa ili kuusafirisha kwenda Ngomeni, mkoani Tanga, kwa ajili ya maziko yatakayofanyika kesho Alhamisi, Aprili 23, 2026.¬