KUNA presha imeshushwa pale Yanga baada ya kurejea kwa mastaa muhimu wawili ambao walikuwa nje kwa sababu mbalimbali, huku kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves akifichua kwamba kutachangamka muda si mrefu.
Iko hivi; kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra amemaliza adhabu yake ya kusimamishwa mechi tatu lakini kama haitoshi, mshambuliaji Prince Dube amerejea rasmi na anaweza kucheza dhidi ya Mbeya City, huku Laurindo Aurellio ‘Depu’ yupo njiani kurejea.
Yanga Alhamisi hii itakuwa nyumbani ikiwakaribisha Mbeya City ambayo ilikuwa timu ya kwanza kupunguza pointi za mabingwa hao watetezi msimu huu, ilipolazimisha sare ya 0-0 zilipokutana duru la kwanza kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pedro alisema baada ya kuumia kwa Aboutwalib Mshery, taarifa njema kwake ni kurejea kwa Diarra ambaye amemaliza adhabu yake iliyotokana na kumfanyia vurugu mwamuzi, wakati Yanga ikicheza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.
Pedro alisema, Diara ni mchezaji muhimu ambapo anaamini atarudi akiwa tayari kuendeleza ubora wake kwenye mechi zijazo kuanzia dhidi ya City.
“Ndio Diarra amerudi, ni taarifa njema, kama unavyofahamu kabla ya kucheza na Pamba kule Mwanza, kipa wetu Mshery alipata maumivu ya goti, tukabaki na Masalanga (Hussein) pekee na kipa wa timu ya vijana,” alisema Pedro.
“Kurudi kwa Diarra ni taarifa njema kwetu, amemaliza adhabu yake, sitaki kurudia nini kilisababisha tukio lile, lakini siku zote ni furaha unapoona mchezaji wako anayetamani kushinda wakati wote na kiongozi muhimu uwanjani anarejea kazini.”
Mbali na Diarra, Pedro alisema Dube aliyerejea mechi iliyopita dhidi ya Pamba Jiji na kucheza kwa dakika 14, dhidi ya Mbeya City matumaini yake ni kumuanzisha, huku Depu akisubiri kidogo kukaa sawa kiafya.
Dube alipata shida ya misuli wakati Yanga ilipokuwa inacheza ugenini dhidi ya TRA United akikosa mechi nne huku Depu akichana nyama za paja ambapo naye alikosa mechi tano.
“Nina matarajio makubwa baada ya urejeo rasmi wa Prince Dube, mchezo uliopita alipata dakika 14 baada ya kutoka kwenye majeraha, ujio wake utaongeza nguvu na ufanisi kwenye eneo la ushambuliaji. Bado Depu hajaanza kurejea uwanjani, hivyo kurejea kwa Dube kutaleta matumaini makubwa kwetu. “Tunaratajia kumkosa Mwanengo (Emmanuel) pia, lakini ni kazi yetu kama benchi la ufundi kutafuta njia mbadala ya kuziba pengo la majeraha.”
Akizungumzia mechi dhidi ya Mbeya City, Pedro alisema: “Mchezo wa mwisho nilifanya mabadiliko kadhaa ili kutoa fursa kwa baadhi ya wachezaji kupata utimamu wa kimwili, ulikuwa wasaa mzuri pia kupumzisha baadhi ya nyota wetu. Hivyo nina matarajio hapo kesho (leo) kuwa ufanisi wa wachezaji wangu utakuwa mkubwa na malengo yetu ni kupata alama tatu pamoja na kutoa burudani kwa mashabiki wetu.
“Mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Mbeya City ulikuwa mchezo mgumu sana kutokana na hali ya uwanja, kesho (leo) tutacheza kwenye mazingira tofauti ambayo tumeyazoea. Nakiri sisi tupo imara zaidi na tunauhitaji mkubwa wa alama tatu. Nafahamu hata wao wanahitaji alama lakini kwetu ni hadithi nyingine, ninajiamini kwa kiwango kikubwa kuwa timu yangu ipo kwenye ufanisi mzuri sana wa kimbinu na kiufundi.
“Licha ya kwamba tunahitaji alama tatu kwa namna yoyote ile lakini tunapaswa kuwa na tahadhari. Lazima tuwaheshimu wapinzani wetu. Mbeya City wana kikosi kizuri chenye uzoefu mkubwa. Umakini ndio nguzo yetu kwa hapo kesho. Mpira ni mchezo wa makosa ukifanya kosa moja linaweza kugharimu mchezo mzima.”
Kwa upande wa Kocha wa Mbeya City, Mecky Maxime, alisema: “Tunajua tuna mchezo dhidi ya Yanga, timu inayoongoza ligi, tumetoka kucheza michezo migumu dhidi ya KMC, Azam na Singida, kesho (leo) ni dhidi ya Yanga, kwa hiyo nafikiri kila mechi ina aina yake ya kuingia.
“Italeta presha sana kutokana na nafasi tuliyopo, lazima tuingie kwa umakini, tumuheshimu mpinzani, kwa sababu ni mechi ngumu, hivyo mechi ngumu lazima zichezwe kwa umakini.
“Tumejiandaa vizuri na hiyo mechi, tumefanya mazoezi vizuri, naamini utakuwa mchezo mzuri.”
Mbeya City ambayo imewahi kupata ushindi mara moja pekee dhidi ya Yanga katika ligi zilipokutana Novemba 2, 2016, huku ikipoteza 11 na sare tisa, Maxime alisema: “Mimi naamini kwenye mpira hamna historia, mpira ni mchezo ambao unachezwa siku husika, inategemea wachezaji wako wameamka namna gani na wako nafasi gani.
“Unajua wakati mwigine hizi timu zinapata presha kutokana na matokeo waliyokuwa nayo. Kikubwa ni mwalimu umepangaje mpango kazi wako na utacheza vipi, wachezaji wanapaswa kuvumilia kwa sababu unapokuwa timu ya pili sio rahisi, lazima uwe fiti na uvumilie kwani mpinzani atakushambulia sana, kubwa zaidi wachezaji wakiwa ‘smart’ unalipata lile unalolitaka.”
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara, Yanga imebakisha mechi 12 ili kukamilisha msimu wa 2025-2026 na ikiwezekana itetee ubingwa inaoushikilia kwa misimu minne mfululizo.
Katika mechi hizo 12 zilizobaki, Yanga inahitaji kutopoteza 11 tu ili kufikia rekodi tangu iliyoweka misimu mitatu iliyopita ilipocheza jumla ya mechi 49 bila kupoteza.
Kama itacheza mechi zote 12 zilizosalia bila kupoteza, basi itarejea kile ilichofanya msimu wa 2021-2022 ilipotwaa ubingwa kibabe bila kupoteza.
Kama hujui, hivi sasa Yanga imeshafikisha jumla ya mechi 38 bila kupoteza, ikiwa ni mechi 11 nyuma ya zile ilizofikisha kutoka Aprili 25, 2021 hadi Novemba 29, 2022 kabla Ihefu SC sasa Singida BS kuwatibulia kwa kichapo cha mabao 2-1.
Mara ya mwisho kwa Yanga kuonja kipigo katika Ligi Kuu ilikuwa ni Novemba 7, 2024 iliponyukwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani na Tabora United, sasa TRA United.
Mara baada ya kipigo hicho kilipopatikana katika mechi ya 10 ya msimu uliopita, Yanga imeunganisha kwa kugawa dozi au kutoka sare katika mechi 20 za kumalizia msimu huo na 18 za msimu huu.
Kwa sasa imesalia na mechi 12 za kufunga msimu ili iue ndege watatu kwa jiwe moja, yaani kubeba taji kwa msimu wa tano mfululizo, kumaliza msimu bila kupoteza na kuifikia rekodi ya kucheza mechi 49 za ligi mfululizo bila kupoteza iliyoiweka misimu mitatu iliyopita Hata hivyo, Yanga ni lazima ijipange kweli kweli kwani ratiba iliyonayo na vigogo atakavyokutana navyo katika mechi hizo 12 zilizosalia sio mchezo.
Mechi hizo 12 ilizobakiza Yanga ni dhidi ya Mbeya City, Simba, KMC, Coastal Union, Dodoma Jiji, Singida Black Stars, Namungo, Mashujaa, Fountain Gate, Azam, TRA na JKT Tanzania.
MASHUJAA KUJIULIZA KWA SINGIDA BS
Ushindi wa mechi moja pekee dhidi ya Singida Black Stars katika Ligi Kuu Bara, ni kitu kinachowaumiza kichwa Mashujaa wanapokwenda kukabiliana na wapinzani wao hao Alhamisi hii.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara, imepangwa kuchezwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo Mashujaa itakuwa mwenyeji.
Rekodi zinaonyesha kwamba, Mashujaa mara ya kwanza kukutana na Singida, iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 tena ikiwa nyumbani, baada ya hapo, haikuwahi kushinda zaidi ya kupoteza na kutoka sare.
Msimu uliopita, ilishuhudiwa Singida ikiichapa Mashujaa mechi zote mbili, ikianza na ushindi wa bao 1-0 ugenini, kisha nyumbani ikashinda 3-0 na msimu huu pia ikashinda 1-0 nyumbani.
Matokeo ya mechi hizo tatu za mwisho, ni mtihani kwa Kocha wa Mashujaa, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kuhakikisha vijana wake wanatikisa nyavu za wapinzani na kuondoka na ushindi kwani huko nyuma wameshindwa kufanya hivyo, tangu mara ya mwisho wapate mabao matatu dhidi ya Singida waliposhinda 2-0 (Septemba 16, 2023), kisha 1-1 (Februari 28, 2024).
Muhibu Kanu ambaye amekabidhiwa kijiti cha kuiongoza Singida Black Stars akiwa na Papy Kimoto, nao wana kazi ya kufanya kulinda nidhamu ya ushindi ugenini kwani msimu huu katika mechi tisa ilizocheza, imepoteza moja, sare nne na kupoteza idadi kama hiyo.
Mkazo huo wa Singida unatokana na wenyeji wao Mashujaa msimu huu kutopoteza mechi nyumbani katika ligi ikishinda tatu na sare sita. Ni miongoni mwa timu zenye rekodi hiyo ya kutopoteza nyumbani sambamba na Yanga na Azam.
