Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo amehimiza ushirikiano wa karibu kati sekta ya umma na binafsi kwa sababu ndiyo watekelezaji wakuu wa mipango ya maendeleo.
Waziri Kitila amefafanua kuwa sekta ya umma na binafsi ni timu moja inayosaka ushindi wa kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 16, 2026 wakati akikazia mambo muhimu baada ya kuwasilisha makadirio ya bajeti ya Sh1.792 trilioni akiliomba Bunge kumuidhinishia ili akatelekeze vipaumbele vitano kwa mwaka 2026/27.
“Ushindi wa timu moja unategemea ushirikiano wa uwekezaji, hivyo ni muhimu kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi katika malengo yetu ya kiuchumi,” amesema.
“Tuwe na lengo na juhudi za pamoja, tukiwa na sauti moja, tutakuwa wimbo mzuri wenye mfumo wa sekta ya umma na binafsi,” amesema Kitila.
Mbali na hilo, Profesa Kitila amesema ni muhimu kujenga uthubutu wa kujaribu mambo mapya na kujenga utamaduni pamoja nidhamu ya kutenda.
Kutokana na hilo, Waziri Kitila ametaka wanaofanya mambo mapya kulindwa na kuthaminiwa.
Amesema dhima ya uongozi walionayo hatimaye ni maendeleo ya uchumi na maisha ya Watanzania, hivyo kila hatua wanayoichukua au nadharia wanayoifikiria lazima ilenge kuboresha uchumi na maisha ya wananchi.
“Katika kupima mafanikio ya mipango tulionayo, tutazingatia vigezo vya kukuza uchumi, kuboresha maisha ya watu, kupungua kwa umasikini, kuongezeka kwa ajira hasa vijana,” amesema Profesa Kitila.
