Baba alivyoua mke mkubwa, mtoto kwa kuwanyonga

Arusha. Ni ukatili, wivu au tatizo la afya ya akili? Ni swali ambalo unaweza kujiuliza pale mauaji ya kikatili yanapojitokeza katika familia, kama tukio la Shamsudin John la kumuua mke mkubwa na mwanae kwa sababu ya wivu wa mapenzi.

John alimuua mkewe Asia John au Selina Tulway kwa kumnyonga kwa kanga, kisha akachukua mwili wake na kuuzika nyuma ya nyumba aliyokuwa akiishi na mke mdogo.

Kwa kuwa mtoto wake, Ahmed Shamsudin alikuwa analia kwa sauti kutokana na kushuhudia kile baba alichokifanya kwa mama yake, baba huyo aliamua kumnyonga naye kwa mikono yake kisha kuutumbukiza mwili wake kwenye bwawa.

Mauaji hayo yalitokea Oktoba 31, 2018 katika Kijiji cha Hideti kilichopo katika Kata ya Hideti katika mji wa Kateshi Wilaya ya Hanang.

Simulizi hiyo imo kwenye hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania iliyotolewa Aprili 15, 2026 na jopo la majaji watatu waliobariki adhabu ya kifo, iliyotolewa na Jaji Devotha Kamuzora kwa Shamsudin John Desemba 7, 2022.

Majaji hao Shaban Lila, Patricia Fikirini na Sam Rumanyika, wamesema licha ya kuufuta ushahidi wa shahidi namba moja, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mwanzo Kateshi, Claudia Tamanu, ushahidi uliobaki jaladani bado unamtia hatiani mtuhumiwa.

Shahidi huyo ndiye aliyeandika maelezo ya ungamo, ambayo yalipokewa kama kielelezo P1 cha upande wa mashitaka, na katika maelezo hayo, mrufani alidaiwa kusimulia hatua kwa hatua jinsi mauaji hayo yalivyofanyika.

Majaji hao walikubaliana na sababu ya pili ya rufaa ya John, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikosea kisheria na kiushahidi, alipomtia hatiani kwa kuegemea maelezo hayo yaliyochukuliwa pasipo kufuata mwongozo wa Jaji Mkuu.

Sababu nyingine mbili za rufaa, akidai Jamhuri ilishindwa kuthibitisha shitaka pasipo kuacha mashaka na kushindwa kuzingatia ushahidi kwamba Asia aliuawa kwa kanga lakini khanga hiyo haikutolewa kama kilelezo.

Hata hivyo, majaji hao walitupilia mbali sababu hizo na kueleza kuwa hata pale ambapo unakosekana ushahidi wa shahidi wa kwanza na kielelezo P1; bado ushahidi mwingine ulitosheleza kumtia hatiani na kustahili adhabu aliyopewa.

 “Kwa ushahidi uliopo ni wazi kuwa, wakati Polisi wakiupeleka mwili wa mtoto kituo cha Polisi na baada ya kusogea takriban mita 200, mrufani aliomba gari la polisi lisimame ili aoneshe mahali ulipo mwili wa mkewe aliyefariki.

“Shahidi namba mbili zaidi alisema mrufani alimwambia kuwa, kutokana na wivu wa marehemu, mke mkubwa kutokuwa tayari kumruhusu kuishi na mke mdogo, alimnyonga hadi kufa kwa khanga na baadaye alimnyonga mtoto kwa mikono yake.

“Shahidi huyu anasema mrufani aliongoza gari la polisi hadi nyumbani kwake ambapo aliwapeleka nyuma yake ambapo walikuta miti ya mbaazi, aliwaambia waondoe mbaazi na wakapata mwili wa mke wake.

“Tunahitaji kusisitiza kwamba kile hasa kilitokea kati ya mrufani na polisi watatu ni kwamba, mrufani alitoa taarifa kwa uhuru na kusababisha ugunduzi wa mwili unahusika katika kesi. Yeye kwa mdomo wake alikiri kufanya mauaji hayo.

“Bado tunaona ushahidi uliobaki unatosha kumtia hatiani. Hatuna sababu ya kumkosoa jaji wa mahakama kuu. Tumeridhika bila shaka hukumu ya mrufani katika makosa yote mawili na adhabu iliyotolewa ni halali kisheria,” imesema hukumu hiyo.

Ni kwa msingi huo na kwa ujumla wake, walitupa sababu za rufaa na kusisitiza upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka hayo katika viwango vinavyokubalika na bila kuacha mashaka na hukumu ya kifo aliyopewa ndio inayomstahili.”

Siku ya tukio, saa 11:00 jioni, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Hideti aliyetajwa kwa jina moja la Akweline, alimtaarifu shahidi wa mbili, Idrisa Masawe, ambaye ni ofisa mifugo, kuwa kuna mwili wa mtoto unaelea katika bwawa la maji la Hideti

Kulingana na ushahidi huo, shahidi huyo akaenda eneo la tukio ambapo mwili wa mtoto huyo ulitambuliwa na shahidi namba tatu kuwa ni Ahmed, mtoto wa mrufani na mbali na kuutambua alifichua uwepo wa ugomvi nyumbani kwa mrufani.

Kutokana na taarifa hiyo, shughuli ya kumtafuta mama wa mtoto huyo ilianza bila mafanikio, lakini kukiwa na hisia kuwa huenda naye alikuwa ameuawa ndipo kazi ya kumtafuta mrufani nayo ilianza na alikamatwa saa 12:00 jioni siku hiyo.

Polisi walifika na kumchukua Shamsudin John wakati huo akiwa mshukiwa namba moja, ambapo pamoja na shahidi namba mbili, VEO na shahidi namba tatu, walikwenda hadi nyumba ya mke wake mkubwa (mama Ahmed), lakini hawakumkuta.

Hata hivyo, ndani ya chumba chake, walikuta kinyesi pamoja na matone ya damu.

Polisi waliamua kuupeleka mwili wa mtoto Ahmed Kituo cha Polisi Katesh na baada ya kwenda umbali wa kama mita 200 kutoka katika nyumba aliyokuwa akiishi mke mkubwa, Shamsuduni alimnong’oneza jambo shahidi namba mbili.

Alimuomba awaambie polisi wasimamishe gari ili awaeleze nini kilichotokea, gari lilisimamishwa na ndipo alipowaomba waongozane naye hadi Kijiji cha Orbesh, kilichopo umbali wa kilometa 1.5.

Huko ndipo alipokuwa akiishi na mke mdogo, polisi walikubali na kwenda naye katika kijiji hicho katika nyumba aliyokuwa akiishi na mke mdogo na watoto ambapo walikuta wote wamelala, mrufani aligonga mlango ukafunguliwa.

Hakuwaingiza ndani, badala yake akawapeleka nyuma ya nyumba ambapo walikuta miti ya mbaazi, ambapo iliondolewa na mrufani akawaelekeza wafukue eneo hilo.

Walipofukua kwa kutumia jembe na beleshi huku wakiondoa mchanga kwa mikono, ndipo walikutana na mwili wa mwanamke akiwa amevaa ‘skin tight’ na khanga ambayo ilikuwa imefungwa kwa kukazwa shingoni na mwili huo ulitambuliwa ni wa mkewe, Asia au Selina.

Wakati akiulizwa maswali ya dodoso na wakili Abdallah Kilobwa aliyekuwa akimtetea mrufani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, shahidi huyo alisisitiza kuwa ni mrufani mwenyewe ndiye aliyewapeleka alipomzika mkewe.

Mwili huo ulikuwa haujaharibika na mrufani aliwaeleza, mbele ya askari polisi wanne, kuwa kutokana na wivu wa marehemu kwa kutotaka kumruhusu yeye (mrufani) kuishi na mke mdogo, ndiyo sababu aliamua kufanya mauaji hayo.

Ushahidi unaofanana na huo ulitolewa na shahidi namba tatu kuanzia mwili wa mtoto ulipotolewa katika bwawa, ambaye pia alisema walisikia watoto wakilia katika chumba nyumbani kwa mrufani, ambaye yeye na baba yake walikwenda kufuatilia.

Huko walikuta watoto wa mrufani wakilia huku wakiwa wamefungiwa kwa nje na watoto hao wakawaambia kuwa mama yao ameondoka na baba yao baada ya kutokea ugomvi, walipoingia ndani ndio wakaona matone ya damu.

Shahidi huyo alidai mrufani alikamatwa na baba yake (yaani baba wa shahidi huyo) na katika mahojiano polisi yeye akiwepo, mrufani alidai ni shetani alimwingilia na kusababisha kufanya mauaji ya mke mkubwa na mtoto.

Alipopata fursa ya kuwasilisha utetezi wake kortini, ambao baadaye ulikataliwa na mahakama, mrufani huyo alikanusha ushahidi wa Jamhuri kuwa ni wa uongo na kujiweka mbali kabisa na kifo cha mke wake huyo pamoja na mtoto wake.

Akielezea kifo cha mtoto, mrufani alidai siku ya tukio mama yake alimtuma kwenda kuchota maji katika bwawa la Hideti lakini hakurudi, alimfuatilia na kukuta amezama na kwamba hata juhudi za kumukokoa hazikuweza kuzaa matunda.

Aliamua kumwacha mtoto ili watu wengine watafute njia nyingine za kumuokoa na kwamba alitaka kwenda kumjulisha mkewe, lakini hakufanya hivyo.

Kuhusu kifo cha mkewe, alikanusha kuhusika na kusema kulikuwa hakuna kaburi lolote nyumbani kwake lakini akakiri kuwa Oktoba 31, 2018 alikamatwa na kupelekwa polisi na kwamba mwili wa mkewe aliukuta katika gari la polisi.

Alikana maelezo yake ya onyo aliyoyatoa polisi yaliyopokelewa kama kielelezo P6 kwa maelezo kuwa yalichukuliwa baada ya kuteswa baada ya kupigwa kwa kutumia waya wenye shoti ya umeme ili akubali kutenda makosa hayo.

Pia, alikanusha maelezo ya ungamo aliyoyatoa kwa mlinzi wa amani akisema yalichukuliwa baada ya kuwa polisi wamemtisha asibadili msimamo wa yale aliyoyaeleza polisi na kwamba wakati anayatoa kulikuwa na polisi anasikiliza.

Hata hivyo, baada ya Jaji kusikiliza ushahidi wa pande mbili, alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumhukumu kunyongwa hadi kufa kwa kosa hilo la kuua kwa kukusudia, ndipo akakata rufaa ambayo hata hivyo haikumsaidia, kwani Mahakama ya Rufani imebariki adhabu hiyo.