CRDB Yazindua Msimu wa Pili wa Programu ya Graduate Trainees Kukuza Vipaji vya Vijana

Benki ya CRDB imezindua rasmi msimu wa pili wa programu ya Graduate Trainees, hatua inayolenga kukuza vipaji vya vijana na kuandaa viongozi wa baadaye katika sekta ya fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abdulmajid Mussa Nsekela, amesema CRDB inaendelea kuwekeza kwa vijana wenye uwezo, ubunifu na maono mapana ili kuimarisha uongozi wa sasa na wa siku zijazo.

Amesema programu hiyo ya miaka mitatu inalenga kutafuta na kukuza vipaji kutoka ndani na nje ya nchi, ikiwahusisha vijana kutoka Tanzania pamoja na nchi ambazo benki hiyo inafanya shughuli zake kama Burundi na aq ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pamoja na maeneo mengine kama Dubai.

Kwa mujibu wa Nsekela, zaidi ya maombi 4800 yalipokelewa mwaka huu, lakini baada ya mchakato mkali wa ushindani, vijana 26 pekee ndio waliochaguliwa kuanza rasmi programu hiyo. Alibainisha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na washiriki 18, huku Burundi na DRC zikiwa na washiriki wanne kila moja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utumishi wa benki hiyo, Godfrey Rutasingwa, amesema msimu huu umeleta pamoja vijana kutoka nchi tatu Tanzania, Burundi na DRC ambao wameanza safari ya kukuza uwezo wao kitaaluma na kiutendaji ndani ya benki hiyo.

Aliongeza kuwa huu ni msimu wa pili wa programu hiyo kufuatia mafanikio makubwa ya msimu uliopita ulioshirikisha vijana 30. kutoka nchi hizo, ambao walitoa mchango mkubwa katika kukuza biashara ya benki, hasa kupitia ubunifu katika teknolojia na mifumo ya kompyuta.

Naye mmoja wa washiriki wa programu hiyo, Frank Mukwabe amesema a programu hiyo imekuwa fursa muhimu kwa wahitimu wapya wa vyuo vikuu wanaokosa uzoefu wa kazi wanapoingia kwenye soko la ajira.

“Tunatarajia kupitia programu hii kuzalisha viongozi wa baadaye watakaoleta mageuzi katika sekta ya fedha kupitia teknolojia na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania,” alisema.