Morogoro. Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula amewaomba Watanzania kuwa na imani na wakaguzi wa fedha kwa sababu ni watu waliosomea taaluma hiyo na wanajua nini cha kufanya wanapokuwa kwenye jukumu la kukagua fedha zinazotolewa na Serikali.
Akifungua mkutano wa nne wa wakaguzi wa ndani wa taasisi na sekta za umma uliofanyika leo Aprili 26, 2026 mkoani Morogoro, Luswetula amesema pamoja na kujengewa imani, pia, wakaguzi hao wanapaswa kuwa huru kwa kuwa wao ndio macho ya Serikali kwenye matumizi ya fedha za serikali.
“Mnaweza kuwa mashahuda kwamba ripoti zinazotolewa kila siku na wakaguzi hawa wa ndani utaona kabisa zinalenga katika kufichua maovu na madudu ambayo watu wachache wasiokuwa waaminifu wanatumia fedha zinazotolewa na Serikali kwa matumizi mengine tofauti na matumizi yaliyoidhinishwa,” amesema Luswetula.
Amesema wakaguzi wa ndani wasiingiliwe na mtu yeyote na ikitokea mkaguzi ameingiliwa kwenye uamuzi na akakubali, jambo hilo basi naye atakuwa amekwenda kinyume na maadili ya taaluma yake, hivyo hatua zitakuchukuliwa dhidi yake.
Aidha, amesema kuwa jukumu mojawapo la wakaguzi hao ni kuwa tayari kuhakikisha kwamba wanakagua matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenda kwenye taasisi ama miradi ya maendeleo na kutoa majawabu sahihi bila kumuonea wala kumpendelea mtu.
Naibu Waziri wa fedha, Laurent Luswetula akifungua mkutano wa nne wa taasisi ya wakaguzi wa ndani wa sekta za umma ambapo amesisitiza wakaguzi hao kuwa huru kwa kuwa wao ndio macho ya Serikali katika matumizi ya fedha kwa mashirika ya umma na miradi ya maendeleo. Picha Hamida Shariff
“Serikali ipo tayari kuwaunga mkono katika kazi zenu ili kuhakikisha mnafanya kazi katika mazingira yenye uhuru na yasiyo na vitisho na endapo patatokea mwingiliano katika majukumu yenu, muwe huru kutoa taarifa ili kupata ufumbuzi na utatuzi wa jambo husika,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani, Jonathan Ngoma amesema kukosekana kwa uhuru kwa baadhi ya wakaguzi ndiko hasa kunakosababisha kuendelea kuwepo kwa upungufu wa kiutendaji.
“Mkaguzi yeyote anatakiwa awe huru, aseme hapa kuna matatizo, lakini usipokuwa huru hutaweza kuyasema matatizo unayoayaona na ndio maana tumekuwa na matatizo amabyo hayaishi, au mwingine anayaona halafu wewe huayaoni na wakati mwingine akiyaona ataambiwa liache kama lilivyo, matokeo yake matatizo yataendelea kuwepo,” amesema Ngoma.
rais na Mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya ukaguzi wa ndani, Jonathan Ngoma akitoa taarifa ya utendaji kazi wa bodi hiyo kwenye mkutano wanne wa wakaguzi wa ndani wa sekta na taasisi za umma uliofanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Mecklaud Edson, mkaguzi mkuu wa ndani katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, amesema katika matumizi ya fedha kwa mashirika ya umma na miradi ya maendeleo, anaamini kupitia maboresho ya sheria ya fedha yaliyofanyika mwaka 2025 yataongeza ufanisi katika kaguzi za mwaka ujao wa fedha.
Naye, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Muhammad Ibrahim amesema mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kuzitambua mbinu za ukaguzi zitakazowasaidia kwenye kazi zao za ukaguzi.
Amesema masuala ya kiutawala yanapaswa kupewa kipaumbele na kuwekewa mkazo katika taasisi za umma hasa zile zinazohusika katika masuala ya uwekezaji moja kwa moja pamoja na zenye bodi za wakurugenzi ili kuleta chachu na kutafikia malengo husika.
