MAANDALIZI ya mashindano yanayosubiriwa kwa hamu ya Kombe la Muungano yamezidi kushika kasi kufuatia kuthibitishwa kwa timu zote nane zitakazoshiriki.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Aprili 21 hadi 29, mwaka huu yakichezwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, yanasubiriwa kutoa ushindani mkali kati ya klabu bora kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai, alisema kuwa uzinduzi rasmi wa mashindano hayo utafanyika Ijumaa saa 4:00 asubuhi jijini Dar es Salaam, katika ukumbi utakaotangazwa baadaye, huku timu zote tayari zikiwa zimethibitisha ushiriki wao.
Mabingwa watetezi Yanga wataongoza timu za Tanzania Bara, wakifuatana na Simba, Azam na Singida Black Stars. Kutoka Zanzibar zitakuwepo KVZ, Muembe Makumbi, Mlandege na Mafunzo, huku waandaaji wakiamini kutakuwa na ushindani mkubwa.
Vuai alisema hafla ya uzinduzi inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi waandamizi wa serikali, wakiwemo mawaziri wa michezo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni.
Aliongeza kuwa uzinduzi huo pia utahusisha zoezi la kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha bajeti ya mashindano hayo inayofikia Sh1.02 bilioni.
“Tunaalika wadau wote wa soka, wakiwemo taasisi za serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na mashabiki, kuunga mkono mashindano haya. Bajeti hii itagharamia mahitaji mbalimbali ya maandalizi ili kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kitaalamu,” alisema Vuai.
Alifafanua kuwa, fedha hizo zitagharamia zawadi kwa washindi, tuzo binafsi kama mchezaji bora wa mechi, malazi kwa timu zinazoshiriki, usafiri pamoja na gharama nyingine za uendeshaji wa mashindano.
Kwa mujibu wa Vuai, tayari shirikisho limeongeza juhudi za kutafuta wadhamini kwa kuwasiliana na wadau mbalimbali kutoka sekta tofauti. Alisema barua rasmi zilizoidhinishwa na serikali tayari zimetumwa kwa wadhamini watarajiwa ili kukusanya fedha zinazohitajika.
“Tayari tumewasilisha barua kwa wadhamini kadhaa na tunaendelea kuwafikia wengine. Mashindano haya yanahitaji ushirikiano wa pamoja, na tunaamini wengi watajitokeza kuunga mkono,” alisema.
Kombe la Muungano linatarajiwa kuwakutanisha baadhi ya vipaji bora vya soka katika ukanda huu, ikiwa na uwakilishi sawa wa timu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, jambo litakaloleta ushindani wenye uwiano na utofauti.
Vuai alieleza matumaini kuwa toleo la mwaka huu litakuwa na ushindani mkubwa zaidi kuliko yaliyopita, akitaja ubora wa timu zinazoshiriki pamoja na maandalizi yao.
“Mashindano haya yanaendelea kukua kila mwaka. Kwa timu tulizonazo safari hii na maandalizi yao, tunatarajia ushindani mkubwa na burudani kwa mashabiki,” alisema.
Mshindi wa mashindano hayo anatarajiwa kujinyakulia kitita cha kati ya Sh100 milioni hadi Sh150 milioni, hatua inayolenga kuongeza hamasa kwa timu pamoja na kuinua hadhi ya mashindano.
Huku timu zote zikiwa zimethibitishwa na maandalizi yakiendelea vizuri, sasa hesabu ya kuelekea kuanza kwa mashindano hayo ambayo bingwa mtetezi ni Yanga, imeanza rasmi.