Azam FC yamsaka mbadala wa Kitambala

Azam FC ipo kwenye harakati za kusaka straika ikielezwa uamuzi huo unafanyika kutokana na namba zisizoshawishi za ufungaji mabao wa Mkongomani Jephte Kitambala.

Kitambala aliyetua Azam msimu huu akitokea Union Maniema ya DR Congo ameanza vibaya Ligi Kuu akifunga mabao mawili katika mechi 16 alizocheza sawa na dakika 1,002.

Kiwango cha mshambuliaji huyo kimeonekana cha kawaida huku akifunikwa na Mkongomani mwenzake, Jean Ngita aliyetua dirisha dogo akiwa na mabao manne katika mechi saba za ligi.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimedaihuu unaweza kuwa msimu wa kwanza na mwisho kwa Kitambala kwani mshambuliaji huyo hajatimiza matarajio ya mabosi.

“Uwezekano wa kubaki kwa Kitambala ni mdogo sana, kiwango chake kimekuwa tofauti na matarajio yetu na hata kocha (Florent Ibenge) ambaye kimsingi ndiye aliyemleta amepata shida na ameomba tutafute mshambuliaji mwenye ufanisi bora zaidi yake.

“Tumekuwa tunazungumza naye sana na hata benchi la ufundi nalo limefanya hivyo, lakini hatuoni mabadiliko, unaona sasa ameshazidiwa mabao hata na Ngita ambaye alikuja baadaye.

“Bado hatujapata nani mbadala wake, lakini kuna majina tunayafuatilia ikiwezekana msimu ujao tuwe na mshambuliaji mkubwa na bora zaidi, ukiangalia msimu huu hilo ni eneo ambalo limetupa shida sana tutatulia tupate mtu au watu sahihi,” kilisema chanzo hicho.

Licha ya rekodi za washambuliaji kuwa chini kwa upande wa Azam, lakini kwa viungo mambo ni tofauti kwani anayeongoza kwa mabao mengi ni Feisal Salum akiwa nayo saba katika mechi 16 alizocheza.

Mpaka sasa Azam imeshacheza mechi 18, ikishinda nane, sare 10 ikiwa haina rekodi ya kupoteza mchezo hata mmoja, ikifikisha jumla ya poiti 34 na kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.