Global Publishers
April 17, 2026
0 Comments
Klabu ya Mbeya City imetangaza kuachana na Kocha Mkuu wake, Mecky Maxime, pamoja na benchi lake la ufundi kwa makubaliano ya pande zote, kufuatia matokeo mabaya ya hivi karibuni ya timu hiyo.
Mbali na Maxime, wengine walioondoka ni Kocha Msaidizi Nizar Khalfan na Kocha wa Utimamu wa Mwili, Francis Mkanula. Uamuzi huo umefikiwa saa chache tu baada ya Mbeya City kupokea kipigo kizito cha mabao 6-0 kutoka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Young Africans SC, katika mchezo uliopigwa katika dimba la KMC Complex.

Kupitia taarifa rasmi, uongozi wa klabu hiyo umeeleza kuwa unathamini mchango mkubwa uliotolewa na Maxime na benchi lake katika kipindi chote walichohudumu, huku ukiwatakia kila la heri katika hatua zao zijazo.
Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa mabadiliko mapya ndani ya Mbeya City, huku mashabiki wakisubiri kuona nani atakayerithi mikoba ya benchi la ufundi na kuiwezesha timu kurejea katika kiwango bora cha ushindani.
