Wataalam kutoka Makumbusho ya Taifa la Tanzania wametoa mafunzo ya kizalendo kwa washiriki wa shindano la Urembo wa Dunia, Tanzania (Miss World Tanzania 2026) katika ukumbi wa White Sand Resort, tarehe 16/04/2026 ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa kuhusu Utalii, historia, utamaduni na urithi wa Taifa.
Katika mafunzo hayo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na wakufunzi hao kwa lengo la kuwawezesha washiriki kuitambua historia yao na kuwa mabalozi bora wa utamaduni wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
Afisa Utalii, Bw. Chance Ezekiel aliwasilisha mada kuhusu Utalii wa Tanzania, akieleza kwa kina hatua za maendeleo ya sekta hiyo na kutoa mwelekeo wa kitaifa kuhusiana na tasnia nzima ya utalii na ubalozi wake hapa Tanzania.
Kwa upande wa Wahifadhi Historia, Bw. Nasri Omari alitoa mada kuhusu historia ya Makumbusho ya Taifa kwa kutolea ufafanuzi wa mamlaka na maeneo ya kiutawa ya taasisi pamoja na vituo na Malikale zinazosimamiwa nayo. Naye Bw. Shomari Rajabu alijikita katika kuelezea maadili, mila na namna bora ya kuzungumza na jamii ili kuendeleza na kulenga kuwa mabalozi bora wa Tanzania.
Washiriki wa Miss World Tanzania 2026 walionesha kufurahishwa na mafunzo hayo, wakibainisha kuwa yameongeza maarifa na uelewa wao kuhusu Utalii, historia, mila na desturi za Mtanzania.
Makumbusho ya Taifa inaendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa elimu kwa umma kuhusu uhifadhi na uendelezaji wa urithi wa taifa kupitia programu mbalimbali za elimu na mafunzo.
.jpeg)


