Unguja. Wakati kukiwa na ongezeko la mahitaji za kugharamia miradi ya kimkakati, imeelezwa kuwa mawakili wa Serikali wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa sheria za kimataifa, mikataba ya kifedha na mbinu za majadiliano wakati wa kuingia mikataba ya mikopo ili kulinda maslahi ya taifa.
Tofauti na mikopo ya masharti nafuu, mikopo ya kibiashara huja na vigezo na viwango vya kibiashara vinavyoendana na soko, masharti ya ulipaji yenye ukomo na uwajibikaji mkubwa na mara nyingi huambatana na masharti ya kisheria yenye uzito mkubwa.
Hayo yamebainika leo Aprili 17, 2026 wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa mawakili wa Serikali ya Zanzibar kuhusu masuala ya kisheria katika mikopo.
Katika hotuba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk Mwinyi Talib Haji ya kufungua mafunzo hayo iliyosomwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Shaaban Ramadhan Abdalla alipomwakilisha, amesema mikopo hii huhitaji umakini wa hali ya juu katika maandalizi, majadiliano na utekelezaji wake.
“Lengo kuhakikisha kuwa Serikali haiingii katika mikataba itakayopelekea kudumaza uchumi wa nchi kwa muda mrefu,” amesema.
Dk Talib amesema matumizi ya dhana ya mikataba ya mikopo katika nyanja ya kimataifa, yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, hasa katika ufadhili wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nane, kumekuwapo ongezeko la mahitaji ya rasilimali za kifedha kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, bandari, viwanja vya ndege na vituo vya afya.
Ili kukabiliana na mahitaji ya kifedha, Serikali imekuwa ikitumia mbinu za upatikanaji wa fedha, ikiwemo utaratibu wa kupata mikopo ya kibiashara.
Mikataba ya aina hii mara nyingi huandaliwa kwa kufuata viwango vya kimataifa na hujumuisha vipengele muhimu ikiwemo sheria itakayotumika, utaratibu wa utatuzi wa migogoro hususani kupitia usuluhishi wa kimataifa, dhamana za Serikali na mgawanyo wa hatari kati ya wahusika wa mkataba.
“Kutokana na upekee huo, ni dhahiri kwamba mawakili wa Serikali wanapaswa kuwa na uelewa mpana wa sheria za kimataifa, mikataba ya kifedha, pamoja na mbinu za majadiliano kwa ajili ya kulinda maslahi ya taifa katika mikataba hii,” amesema Dk Talib.
Kwa kuwa utaratibu mzima wa kupata mikopo unahusisha mikataba mikubwa baina ya Serikali na wakopeshaji, amesema hali hii inaweka wajibu mkubwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu pamoja na mawakili wa Serikali kwa ujumla, kuhakikisha mikataba yote inafanyiwa uchambuzi wa kina wa kisheria kabla ya kutiwa saini kwa ajili ya utekelezaji wake.
Kadhalika, amesema mawakili wa Serikali wanatakiwa kuhakikisha maslahi ya Serikali yanalindwa kikamilifu, kuhakikisha kuwa masharti ya mikataba ni ya haki, wazi na yanayotekelezeka na hatari zote zinazoweza kujitokeza zinatambuliwa mapema na kudhibitiwa ipasavyo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Sheria wa CRDB, Pascal Mihayo amesema wamekuwa wakifanya miradi mikubwa kwa ushirikino na serikali kufanikisha mikopo hiyo.
“Tumekuwa tukifanya mikopo hii na serikali chini ya mwanasheria mkuu, lakini kutokana na uzoefu muda mrefu, kwa hiyo tumeona ni vyema kuweka mafunzo na majadiliano namna tunavyoweza kusaidiana katika kuingia mikataba,” amesema Mihayo.
Amesema katika mafunzo hayo wameangalia zaidi ni kinafanyika na kuendelea kabla wakati na baada ya kuingia mikataba.
“Ukishasaini mkataba sio kwamba unuchukua na kuuweka kabatini, kuna wajibu kuna mambo amabyo pande mbili zinatakiwa kufuatilia na madhara yake ndio maana tumekuja kukaa kubadilisha uwezo,” amesema.
Amesema awali mikataba ilikuwa inaweza kuchukua hadi miezi sita mpaka kumaliza lakini bada ya mafunzo hayo wanatarajia itafupishwa muda ili seriklai ipate fedha haraka kwa ajili ya maendeleo.
Amesema mikataba ambayo ni dhaifu serikali inaweza kupata hasara kwani umuhimu wa mkataba ni kuuangalia kabla ya kuingia kwani inatakiwa kuhakikisha wanalinda maslahi yao.
Naye, Meneja wa CRDB Tawi la Zanzibar, Fatma Nassor amesema watafungua fursa nyingi kwani mambo ya sheria yakiwa sawa hata biashara
“Kupitia warsha hii itatupa fursa nyingine kupata miradi ya kimakakti ya serikali na sisi tupo tayari kuta ushirikiano kuhakikisha kwamba nchi yetu inaendela kuzingatia misingi ya kisheria,” amesema