MAMBO manne yanaupa uwanja wa AFCON 2027 unaojengwa Arusha utofauti na viwanja vingine vinavyotumika kwa mechi za soka na michezo mingine hapa nchini.
Uwanja huo ambao kwa sasa ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 60, ni miongoni mwa viwanja vilivyopangwa kutumika kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.
Meneja Mradi wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China (CRCEG) inayojenga uwanja huo, Dennis Mtemi amesema hayo katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuwa kuna mambo manne ambayo yatapatikana katika uwanja huo pekee nchini.
Mambo hayo manne ni muonekano, muundo, miundombinu inayozunguka pamoja na usalama wake.
Kwa mujibu wa Mtemi, muonekano wa uwanja huo kwa nje unaakisi vivutio viwili vikubwa vya utalii na alama ya nchi kimataifa ambavyo vinapatikana Kaskazini mwa Tanzania, ambavyo ni madini ya Tanzanite na Mlima Kilimanjaro.
“Tumetumia madini ya Tanzanite na dhahabu katika kusanifu muonekano wa nje wa uwanja na paa yetu tumeisanifu kwa muonekano wa Mlima Kilimanjaro. Uwanja wetu pia una kitu kinaitwa ‘Tourism Integration’ (ujumuishi wa utalii). Tunataka tumtengeneze mteja wetu anapokuja kutazama uwanja, awe karibu na vivutio vingine vya utalii. Mtalii napokuja katika uwanja wetu ana sababu ya kwenda katika vivutio vyetu vingine na kutupa fedha za kigeni na kipato katika taifa,” amesema Mtemi.
Mtemi amesema kuwa upande wa muundo, kutakuwa na maeneo matatu tofauti ya watu mashuhuri ambayo yatawekwa kwa mtindo wa maboksi.
Boksi la kwanza litakuwa moja ambalo litakuwa ni sehemu maalum ya kukaa Rais wa nchi, eneo la pili litakuwa na maboksi nane kwa ajili ya viongozi wengine na pia sehemu ya tatu itakuwa na maboksi 15 ambayo yatakuwa kwa ajili ya watazamaji watakaolipia kiasi kikubwa cha fedha ili kupata huduma za hadhi ya nyota tano uwanjani hapo.
Katika maboksi hayo, kutakuwa na maeneo ya mapumziko na huduma nyingine za kawaida pamoja na vioo vinavyomfanya mtazamaji apate fursa ya kutazama mchezo pasipo muingiliano na mashabiki wa kawaida.
Upande wa miundombinu inayouzunguka uwanja huo, kutakuwa na barabara tatu tofauti zinazoingia na kutoka uwanjani hapo na pia utakuwa na viwanja vitatu vya mazoezi vya nyasi bandia ambavyo vitakuwa pembeni yake.
Mtemi amesema kuwa usalama kwa watazamaji umezingatiwa katika eneo lote la uwanja ambalo litafungwa kamera zaidi ya 200 kwa ajili ya kufuatilia kila kinachoendelea uwanjani hapo kabla, wakati na baada ya mchezo.
Meneja huyo miradi ameongeza kwamba ujenzi wa uwanja huo umefuata vigezo vya kundi namba nne la viwanja vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Mkuu aliagiza kuwapo kwa uharakishwaji wa mradi huo pamoja na matumizi stahiki ya fedha za ujenzi wa uwanja huo.
“Kaguzi zitakuja mapema zaidi ya hapa. Fanyeni kazi usiku na mchana. Tusiweke dosari ambazo hazihusiani na maandalizi ya viwanja. Ongezeni vitendea kazi, ongezeni nguvu kazi ili tutekeleze mapema huo muda ambao tumeuweka. La pili tuendelee kuzingatia thamani na viwango vya fedha. Tutimize mahitaji na matakwa ya waendesha shughuli wa AFCON lakini lazima tuwape thamani ya viwango Watanzania ambao ndio watoa fedha ya ujenzi,” amesema Mwigulu.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema uwanja huo utakuwa na vitu vingi vya kuufanya uwe miongoni mwa viwanja bora Afrika.
“Utakuwa miongoni mwa viwanja vitatu bora Afrika vinavyoonyesha uhalisia wa maisha na jiografia ya Afrika. Viwanja vyetu vingi tulivyonavyo havina sehemu ya watu mashuhuri. Mtu kama Rais ni kiongozi mkubwa. Uwanja huu umemtambua na kumpa nafasi yake.
“Kuna vyumba 15 maalum vya VIP ambavyo tutavitoa kwa kuvipa majina ya viongozi wetu waliofanya kazi iliyotukuka katika nchi hii ya Tanzania.
“Mzee wetu Molinge Edward Sokoine lazima jina lake liwepo mahala pale kama sehemu ya watu waliojenga kumbukumbu katika mkoa wetu wa Arusha,” amesema Makonda
