Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ismani, mkoani Iringa na madiwani 12 katika kata mbalimbali utafanyika Juni 1, 2026.
Uchaguzi wa mbunge katika jimbo hilo unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na William Lukuvi ambaye alifariki dunia Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla moyo.
Lukuvi alikuwa ameliongoza jimbo hilo kwa miaka 31 tangu 1995. Wakati anafariki dunia alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge na Uratibu.
Taarifa ya INEC, iliyotolewa leo Jumatatu Aprili 20,2026 na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima imeeleza mbali na uchaguzi huo wa ubunge, pia kutafanyika uchaguzi wa madiwani 12 katika kata mbalimbali nchini.
Kailima amesema kati ya kata 12 zitakazofanya uchaguzi kata 11 madiwani wake wamefariki dunia na mmoja pekee akipoteza sifa za uanachama katika Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.
Kailima kupitia taarifa hiyo amefafanua kuwa fomu za wagombea za uteuzi zitaanza kutolewa Mei 4-10, 2026, uteuzi ukifanyika siku ya mwisho ya uchukuaji na urejeshaji ambayo Mei 10, 2026. Amesema kampeni zitaanza Mei 11-31, 2026 na uchaguzi wenyewe katika kata na Jimbo la Ismani itakuwa Juni 1, 2026.
