Dar es Salaam. Wakati ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam ukitajwa kuongezeka, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametaja changamoto kubwa ya bandari hiyo ni uwepo wa mifumo tofautitofauti ya taarifa akisema hilo linashughulikiwa.
Amesema kwa sasa Kampuni ya DP World wana mifumo yao na Kampuni ya Adan nao wana mifumo yao hivyohivyo kwa taasisi zingine, akisisitiza uwepo wa mfumo mmoja wa taarifa ukiwa ni utekelezaji wa mkataba wa Shirika la Meli Duniani (IMO) utaongezea ufanisi zaidi wa bandari hiyo.
Kulingana na mkataba wa IMO, nchi wanachama wa shirika hilo ikiwemo Tanzania, wanapaswa kuwa na mfumo mmoja wa taarifa kutoka na kuingia kwa meli bandarini.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Jumatatu, Aprili 20,2026 kwenye mkutano wa kimataifa wa kupeana elimu ya masuala ya usafirishaji ulioandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Meli Duniani (IMO) ukikutanisha mataifa zaidi ya 20 kutoka ndani na nje ya Afrika.
Wataalamu mbalimbali wa bahari wakifuatilia mkutano huo Dar es Salaam leo Aprili 20,2025.
Kuhusu ufanisi wa bandari, Profesa Mbarawa amesema mwaka 2021/2022 mzigo uliohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam ulikuwa tani milioni 18 na hadi kufikia 2024/25 uliongezeka kufikia tani milioni 27.7 na mategemeo ni ifikapo 2030 mzigo ufikie tani milioni 30.
“Lakini bado kuna changamoto ya mifumo kutounganishwa pamoja, DP World wana mifumo yao Adan wana mifumo yao na baadhi ya taasisi zina mifumo yao, sasa mifumo hii inasababisha changamoto za taarifa,” amesema.
“Kuna mkataba wa Shirika la Usafiri wa Majini Duniani ambao unazitaka nchi zote wanachama kuwa na mfumo wa pamoja wa kupeana taarifa za mizigo,” amesema.
Waziri huyo amesema mfumo wa huo wa Tehama ni muhimu kwani unakwenda kuongeza ufanisi kwenye bandari ya Dar es Salaam ambayo zaidi ya asilimia 90 ya mizigo ya Watanzania hupitia hapo.
Amesema kukiwa na mfumo mmoja wa taarifa hata ufanisi wa bandari utakuwa mkubwa kwa watu kufahamu mzigo umeingia muda gani na utatoka muda gani, akidokeza kuwa mkutano huo utawasaidia wataalamu wa kwenda kutekeleza kwa vitendo.
Amesema bandari ya Dar es Salaam inapoongeza ufanisi zaidi sio mizigo ya Watanzania tu itanufaika bali hata ya nchi jirani.
Kutokana na umuhimu wa bandari hiyo, Profesa Mbarawa amesema Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye bandari hiyo kuanzia gati namba moja hadi namba saba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum amesema semina hiyo ya kikanda ni kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kimataifa wa kuwa na njia moja ya kuwasilisha nyaraka za usafirishaji wa njia za bahari.
Amesema mkataba huo unataka nchi wanachama kutokuwa na mifumo tofauti tofauti bali mfumo mmoja wa unaorahisisha biashara ya kuingia na kutoka kwa meli baharini.
“Walioshiriki mkutano huo ni zaidi ya nchi 20 na wabia mbalimbali waliofika kutoa mafunzo juu ya mkataba huo na umuhimu wa utekelezaji wake,” amesema.
Salum amesema kuwa na mifumo mingi baharini huchelewesha utoaji wa mizigo bandarini kwani mtu mmoja anaweza kuzunguka taasisi mbalimbali na nyaraka moja wakati mifumo ingesaidia kuondoa changamoto hiyo.
Naye Mbarouk Jamal amesema kutokana na kila taasisi kuwa na mifumo yake mfanyabiashara hulazimika kupitia sehemu nyingi kupata huduma ileile, jambo ambalo linaongeza gharama na kupoteza muda.
“Hii siyo tu changamoto kwa wafanyabiashara wa ndani, bali pia inaiathiri taswira ya bandari yetu kimataifa. Ninaamini kuwa utekelezaji wa mfumo mmoja wa taarifa kama unavyotakiwa na (IMO) utakuwa suluhisho la kudumu,”amesema.
