Shughuli za uokozi maduara yaliyotitia Geita, zahitimishwa

Geita. Kamati ya uokozi na utafutaji mkoani Geita iliyokuwa ikifanya shughuli za uokozi na utafutaji katika mgodi wa Msasa uliopo Kata ya Runzewe, wilayani Bukombe, imetangaza kuhitimishwa kwa shughuli hizo ikiwa ni zaidi ya wiki mbili tangu kutokea kwa tukio la kutitia kwa maduara katika mgodi huo.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 20, 2026 Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Msaidizi,  Keneth Mwakasitu amesema uamuzi huo ulifikiwa Aprili 10, 2026 na kamati hiyo chini ya mwenyekiti wa kamati ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo.

Mwakasitu amesema shughuli hiyo imefanyika kwa mafanikio makubwa huku akitaja baadhi ya vitu vilivyopatikana kupitia shughuli ni vile ambavyo husaidia kwenye shughuli za uchimbaji, ikiwa ni pamoja na winchi, jenereta na injini.

Aidha ameongeza kuwa vingine vilivyopatikana katika maduara hayo ni vitu vidogovidogo kama bambam vinavyotumika kudrili.

“Nitoe rai kwa migodi mingine watumie mainspekta, wasimamizi na machifu kusimamia usalama, kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama haviwezi kukagua kila duara kila siku, kwa hiyo kupitia hawa ambao tumewaamini tunaomba wakafanye kazi kwa bidii,” amesema Mwakasitu.

Moja ya maduara yaliyotitia Machi 29, 2026 ambapo shughuli za uokozi na utafutaji zilihitimishwa Aprili 10, 2026, zikihusisha maofisa madini, Jeshi la Polisi, Zimamoto na Uokoaji pamoja na viongozi wa mgodi huo

Kuhusu shughuli za uchimbaji katika eneo hilo, Mwakasitu amesema kwa sasa hazijaruhusiwa kuendelea kutokana na timu ya ukaguzi inayohusisha wataalamu kutoka Ofisa Madini mkoa wa kimadini Mbogwe na maofisa usalama na wakaguzi wa mgodi, inaendelea kuangalia maduara mengine ikiwa yapo salama kwa shughuli nyingine za uzalishaji ziweze kuendelea.

Tukio la kutitia kwa maduara kwenye mgodi wa Msasa uliopo kata ya Runzewe wilayani Bukombe, lilitokea Jumapili asubuhi ya Machi 29, 2026 na kuibuka kwa taharuki kwenye jamii hasa mitandao ya kijamii, baada ya kuibuka kwa baadhi ya taarifa zikieleza kuwepo kwa vifo na majeruhi kwa watu waliokuwa katika eneo hilo.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Safia Jongo ametoa taarifa iliyofafanua juu ya kutokuwepo kwa vifo wala majeruhi. Pia Kamanda Jongo amekanusha madai ya kutitia kwa maduara 11 ambapo kupitia taarifa yake kwa umma, amebainisha kuwa maduara yaliyokuwa yametitia yalikuwa manne pekee ambayo yalikuwa hayatumiki baada ya maofisa wa mgodi huo kubaini uwepo wa dalili za hatari.

Katika kuondoa sintofahamu hiyo Machi 30, 2026 Kamanda Jongo aliitisha mkutano wa hadhara katika mgodi huo na kubainisha kuwa, Polisi walilazimika kuwatawanya baadhi ya wachimbaji ili kuepusha madhara makubwa ambayo yangetokea kutokana na baadhi yao kutokuwa na utaalamu katika mambo ya uokozi.

“Wengi wenu kwa umati huu, kila mmoja   alikuwa anataka kuingia kwenye fensi akaokoe, hivi tungeokoa au na sisi tungeishia humo? Kwa   mazingira kama hayo, sisi kama Polisi tunao wajibu wa kuzuia watu wote wasiingie, ili waingie wachache, wafanye kazi kitaalamu kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri,” amesema Kamanda Jongo.