Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiadhimisha Siku ya Ini Duniani, Daktari bingwa mbobevu wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Swalehe Pazi, amesema Serikali bado inaendelea kukusanya takwimu halisi kupitia kambi mbalimbali ili kujua wenye changamoto hiyo.
Ingawa hakuna takwimu kamili, ametoa rai kwa jamii kuhusu umuhimu wa uchunguzi afya zao mapema pamoja na mabadiliko ya mtindo wa maisha ili kupunguza hatari ya kukumbwa na maradhi hayo.
Hata hivyo, Dk Pazi amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzisha huduma ya upandikizaji ini nchini, hatua inayotarajiwa kuboresha upatikanaji wa matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa ya ugonjwa huo na kupunguza utegemezi wa rufaa za nje ya nchi.
Ameyasema hayo leo, Aprili 20, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ini Duniani ambayo hufanyika kila Aprili 19 ya kila mwaka. Katika maadhimisho hayo, huduma za bure za uchunguzi, ushauri na chanjo zinatolewa katika hospitali ya Muhimbili hadi kesho Aprili 21.
“Kambi za uchunguzi zinaendeshwa ili kupata takwimu kwa lengo la kubaini ukubwa wa tatizo na kusaidia Serikali kupanga tafiti na mikakati sahihi.”
“Katika kambi hii, iliyoanza leo hadi kesho hatutarajii idadi kubwa kutokana na rasilimali na muda, lakini angalau watu 500 watapatiwa uchunguzi ndani ya siku mbili,” amesema.
Amesema kuwa matatizo ya ini yanaweza kutibika iwapo yatagundulika mapema. Huku akisema virusi vya homa ya ini aina ya B vina chanjo, huku aina ya C ikiwa na tiba pekee lakini haina chanjo.
“Matibabu ya ugonjwa wa ini yapo, hasa kama utagundulika mapema. Kwa mfano, uvimbe wa ini ukigunduliwa na kuondolewa mapema, unaweza kuzuia hata saratani,” amesema.
Amesema changamoto ya ini inaathiri makundi mbalimbali, ikiwemo wajawazito ambao wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakati wa ujauzito au kujifungua.
“Mtoto aliyezaliwa na mama mwenye maambukizi yupo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa,” amesema.
Amesema makundi mengine yaliyo hatarini ni pamoja na wanaojihusisha na biashara ya ngono, pamoja na watu wanaokunywa pombe kwa muda mrefu hata kwa kiwango kidogo.
“Hakuna kiwango salama cha unywaji pombe; iwe kidogo au kingi, bado kuna hatari,” amesema.
Kuhusu mpango wa upandikizaji ini nchini, amesema maandalizi yanaendelea na ni mchakato mkubwa unaohusisha mafunzo na uwezeshaji wa wataalamu.
“Serikali imejipanga, na wakati ukifika, tutatoa taarifa rasmi,” amesema Dk Pazi.
Amesisitiza kuwa siku ya ini duniani ni muhimu kwa kuwakumbusha Watanzania kujali afya zao, kwani wengi hawafanyi uchunguzi wa mara kwa mara.
“Magonjwa ya ini mara nyingi hayana dalili za awali, na wagonjwa wengi hugundulika wakiwa katika hatua mbaya,” amesema.
Amesema Katika kambi hiyo, wanapima virusi vya aina ya B na kuwashauri wale watakaobainika kuwa na maambukizi, pamoja na kuwapatia matibabu.
“Wale watakaobainika hawana maambukizi watapewa chanjo dhidi ya virusi vya ini aina ya B,” amesema.
“Uzito mkubwa husababisha mafuta kujikusanya kwenye ini, hali inayoweza kulifanya lishindwe kufanya kazi vizuri na kuongeza hatari ya magonjwa kama saratani,” amesema.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka kampuni ya Mega WeCare, Wilson Dibinze, amesema wanaendelea kushirikiana na Serikali kuboresha sekta ya afya, hususan katika mapambano dhidi ya magonjwa ya ini.
Naye mmoja wa wananchi, Abeid Twaha aliyefika hospitalini hapo kwa ajili ya kupima, amesema aliamua kufanya hivyo baada ya kuona matangazo, ili kufahamu hali ya afya yake mapema.
“Nimekuja kupima na kupata ushauri wa jinsi ya kujitunza. Nawahamasisha Watanzania wengine kufanya hivyo,” amesema.
