Vitendo hivi vya uhalifu vitafutiwe mwarobaini

Zanzibar ni visiwa vinavyojulikana kwa misimu yake minne ya hali ya hewa, Kaskazi, Kusi, Kipupwe na Masika ambayo huleta mabadiliko ya joto na mvua kwa nyakati tofauti za mwaka. Hali hii ya asili imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa wakazi wake.

Hata hivyo, katika kipindi cha karibuni, kuna kinachoonekana kama msimu mwingine usiotabirika, msimu wa uhalifu ambao huibuka ghafla, kushamiri kwa muda, kisha kupungua baada ya hatua kali za udhibiti kuchukuliwa.

Tofauti na misimu ya hali a hewa, msimu huu wa uhalifu hauna kalenda maalumu. Huonekana kupotea kwa muda na kuwapa wananchi ahueni ya usalama, lakini hurejea kwa kasi isiyotarajiwa. Kwa miezi kadhaa kabla ya mwezi wa Ramadhani, matukio ya uhalifu hasa unyang’anyi na wizi wa nyumbani, ulipungua kwa kiasi kikubwa.

Hali hiyo iliwapa wananchi matumaini kuwa usalama umeimarika. Hata hivyo, hali imebadilika tena, matukio hayo yameripotiwa kuongezeka, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji ya Unguja.

Kwa sasa, simulizi za uporaji njiani hasa katika maeneo yenye giza, zimekuwa zikisikika mara kwa mara kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vikao vya wananchi.

Wahalifu wanaelezwa kutumia silaha kama mapanga na visu na katika baadhi ya matukio, waathirika hujeruhiwa vibaya. Hali hii imezua hofu miongoni mwa wananchi huku wengi wakiishi kwa tahadhari kubwa.

Baadhi ya malalamiko yanahusisha matumizi ya kumbi za starehe kama maficho ya wahalifu. Inadaiwa kuwa maeneo hayo, hasa yaliyo katikati ya makazi ya watu na yanayofanya kazi hadi usiku wa manane, hutumiwa kupanga au kuratibu vitendo vya uhalifu.

Ingawa hoja hii inahitaji uchunguzi wa kina, inaonyesha jinsi jamii inavyotafuta kuelewa chanzo cha ongezeko la vitendo hivyo.

Ikumbukwe kwamba idadi ya watu Zanzibar imeongezeka kwa kasi kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hali inayoongeza shinikizo katika huduma za kijamii na mifumo ya usalama. Ingawa idadi ya vyombo vya ulinzi imeongezeka, bado changamoto ipo, jambo linaloashiria kuwa tatizo si la rasilimali pekee, bali pia ushirikiano na mifumo ya utekelezaji.

Moja ya sababu zinazotajwa mara kwa mara ni ushiriki mdogo wa wananchi katika kusaidia mapambano dhidi ya uhalifu.

Wananchi wengi wanasema hupoteza imani wanapotoa taarifa kwa vyombo vya dola lakini hazifanyiwi kazi ipasavyo, au wanapowaona watuhumiwa wakirejea mitaani muda mfupi baada ya kukamatwa.

Hali hii hupunguza motisha ya kushirikiana na vyombo vya usalama. Kwa upande mwingine, vyombo vya dola vinaeleza kuwa wananchi wenyewe wakati mwingine hawatoi ushirikiano wa kutosha, hasa inapofika hatua ya kutoa ushahidi mahakamani.

Wapo wanaokwepa kufika mahakamani kutokana na gharama za usafiri na muda wanaopoteza, hali inayowaathiri kiuchumi. Kesi zinapocheleweshwa au kupigwa kalenda mara kwa mara, wananchi hupoteza hamasa ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa haki.

Tatizo la rushwa nalo halipaswi kupuuzwa. Linapotokea katika mifumo ya haki na usalama, huathiri ufanisi wa juhudi za kupambana na uhalifu.

Hata hivyo, wananchi wanapaswa nao kutambua wajibu wao. Ulinzi si kazi ya polisi pekee; ni jukumu la kila raia. Kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi na kushirikiana katika kulinda maeneo yao ni hatua muhimu inayoweza kusaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.

Ili kukabiliana na changamoto hii, kunahitajika mikakati ya muda mfupi na mrefu. Kama ilivyo katika mipango ya maendeleo, mapambano dhidi ya uhalifu yanapaswa kuwa na dira, malengo na tathmini ya mara kwa mara. Miundombinu ya usalama, kama taa za barabarani na katika vichochoro, inapaswa kuboreshwa ili kuondoa mazingira yanayowapa mwanya wahalifu.

Aidha, maeneo yanayojulikana kuwa makazi ya vijana wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya yanapaswa kudhibitiwa kwa umakini, kwani mara nyingi huhusishwa na vitendo vya kihalifu. Hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika, bila upendeleo.

Kwa upande wa mahakama, ni muhimu kuwapo kwa utaratibu wa kusaidia mashahidi, ikiwa ni pamoja na posho za usafiri, ili kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika utoaji wa ushahidi. Vilevile, elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya dola inapaswa kuimarishwa, huku viongozi wa kisiasa wakihamasisha wananchi katika majimbo yao.

Vyombo vya habari navyo vina jukumu la ziada. Badala ya kuripoti matukio ya uhalifu pekee, vinapaswa pia kuelimisha jamii juu ya njia za kujikinga na umuhimu wa mshikamano katika kudumisha usalama.

Kwa ujumla, kupambana na uhalifu kunahitaji juhudi za pamoja. Ni lazima kujenga mfumo unaoaminika, unaoshirikisha wananchi na unaowajibika, ili kuhakikisha kuwa usalama wa watu na mali zao unalindwa kwa ufanisi.