Mbunge wa Viti Maalum, Asha Baraka, amemwomba Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuisaidia Simba SC ili nayo ipate uwanja kama ilivyokuwa kwa watani wao wa jadi, Yanga.
Asha Baraka ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 14, 2026 alipokuwa akichangia Hotuba ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambapo amemwomba kuiga mfano wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda aliyeipa Yanga uwanja licha ya kuwa yeye ni shabiki wa Simba.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, vilabu vyetu vimekuwa vikicheza ligi na mashindano ya Kimataifa na kufanya vizuri kutokana na hamasa hasa ya goli la mama, leo nimemwona Waziri Makonda amekaa hapo, yeye akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa kiwanja kwa Klabu ya Yanga, tunaomba na wewe ufanye hivyo kwa timu ya Simba,” amesema Asha.
Mbunge huyo amesema, Klabu ya Simba imekuwa ikiomba Serikali kwa muda mrefu lakini haijafanikiwa, hivyo akasema licha ya mapenzi ya Dk Mwigulu kwa timu ya Yanga, lakini afanye hivyo kwa Simba.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, fumba macho utupe uwanja na sisi Simba ili uweke kumbukumbu nzuri kwa klabu yetu na mtupatie hati,” amesema Asha.
Juni 15, 2019 katika tukio la Kubwa Kuliko lililoandaliwa na Yanga likiwa na lengo la kuichangia klabu hiyo, Makonda wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, aliikabidhi Yanga kiwanja maeneo ya Kigamboni.
Miaka sita baada ya kutangazwa Yanga kupewa kiwanja hicho maeneo ya Kigamboni, Septemba 14, 2025 katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, neema ikazidi kuwaangukia kufuatia kukabidhiwa rasmi hati ya ongezeko la kiwanja kilichopo Jangwani na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Deogratius Ndejembi, kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo ambao ukijengwa na kukamilika, wamepanga kuutumia kwa mechi za mashindano mbalimbali.
Kwa sasa Simba wana Simba Mo Arena uliopo Bunju ambao wanautumia kwa ajili ya mazoezi.