Singida BS akili yote ipo kwenye mashindano ya CAF

WAKATI Singida Black Stars ikifuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, benchi la ufundi limesema hesabu zao msimu huu ni kupata tena tiketi ya kushiriki michuano ya CAF, huku ikizipiga mkwara Yanga na Simba.

Msimu uliopita, Singida Black Stars ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kumaliza nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 57, ikiungana na Azam FC, huku Yanga na Simba zilizomaliza nafasi mbili za juu zikiwakilisha nchi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, msimu huu Singida wameanza tena kampeni ya kuisaka nafasi hiyo baada ya kufanya kweli kwa kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kufuatia ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mbeya City.

Matokeo hayo yaliifanya timu hiyo kuungana na Yanga, Simba, Azam FC, Coastal Union, Mashujaa, TRA United na JKT Tanzania ambazo zitachuana kuwania kutinga nusu fainali kisha fainali na bingwa ndiye ana tiketi ya kuiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa Singida Black Stars, Muhibu Kanu alisema dhamira yao ni kupata tiketi mojawapo kupitia aidha Ligi Kuu au Kombe la Shirikisho la CRDB kuhakikisha wanawakilisha nchi kimataifa.

Alisema baada ya mchezo dhidi ya Mbeya City, nguvu zinaelekezwa mechi ijayo dhidi ya Mashujaa katika Ligi Kuu Bara, Alhamisi hii mkoani Kigoma kuhakikisha wanashinda na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

“Sisi tunachohitaji ni timu ishiriki kimataifa bila kujali tumepitia Kombe la Shirikisho au Ligi Kuu, kwakuwa mashindano yote hayo ni muhimu kwetu tunataka ubingwa na wachezaji tumewahimiza wapambane,” alisema Kanu.

Alisema licha ya ushindani uliopo Ligi Kuu, lakini Singida BS wanataka nafasi mbili za juu huku Kombe la Shirikisho wakisaka ubingwa na baada ya kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo anataka heshima.

“Mwenyewe nataka heshima, rekodi na historia msimu huu, alisema kocha huyo.