MLANDEGE imeweka wazi dhamira yake ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA Unguja baada ya kufuzu robo fainali kwa ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Inter Zanzibar.
Baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Mlandege ilishinda kwa mikwaju ya penalti na kuwa timu pekee iliyofuzu hatua hiyo kwa njia hiyo tangu kuanza kwa hatua ya 16 bora Aprili 13 hadi 16, 2026.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Sabri China, amesema ushindi huo ni mwanzo wa safari yao ya kusaka ubingwa.
“Tunashukuru kufika robo fainali, lakini hatutaki kuishia hapa. Tunapambana kuhakikisha tunakuwa mabingwa,” amesema.
Aliongeza ushindani ulikuwa mkubwa kutokana na wapinzani wao kujituma zaidi wanapokutana na timu kubwa.
Mlandege, ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2024/25, bado haijawahi kushinda Kombe la FA, hivyo inalenga kuweka historia mpya msimu huu.
Aidha, klabu hiyo inalenga kutumia ubingwa huo kama tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, hususan Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.
