WAKATI Ligi Kuu Bara ikisimama baada ya raundi 19 kuchezwa, hadi sasa timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu zimenolewa na jumla ya makocha 38 kutoka nchi mbalimbali.
Katika kundi hilo la makocha 38, wapo walioondoka kabla ya ligi kuanza, wengine wamehudumu kwa kukaimu nafasi ndani ya muda mfupi, kuna waliopewa mikataba ya muda mrefu ikavunjwa kwa makubaliano ya pande mbili, lakini kuna ambao wanaendelea kuzitumikia timu zao hadi sasa.
Katika kundi hilo la timu 16 za Ligi Kuu, ni Azam, Namungo, Pamba Jiji na JKT Tanzania pekee ambazo hadi sasa zinasimamiwa na makocha walewale walioanza nao msimu huu.
Makocha hao ni Florent Ibenge (Azam), Juma Mgunda (Namungo), Ahmad Ally (JKT Tanzania) na Francis Baraza (Pamba Jiji).
Lakini nyingine 12, zimekuwa chini ya usimamizi wa makocha tofauti 35 tangu msimu ulipoanza hadi sasa.
Simba ndiyo timu ambayo imeongoza kwa benchi lake la ufundi kusimamiwa na idadi kubwa ya makocha msimu huu kulinganisha na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu.
Ilianza na Fadlu Davids ambaye aliondoka kabla Ligi Kuu haijaanza lakini aliiongoza timu hiyo katika Ngao ya Jamii ya kufungua msimu na moja Ligi ya Mabingwa.
Baada ya Fadlu kuondoka, Simba ilimchukua kwa muda Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye ilimpa jukumu la kuiongoza katika mechi moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Kibarua cha Morocco kilipokamilika, Simba ikawa chini ya Selemani Matola katika mechi za Ligi na baadaye ikamuajiri Dimitar Pantev ambaye Desemba 2025 ikaja kuachana naye na kumchukua Steve Barker inayeendelea naye hadi sasa.
Fountain Gate inafuatia kwa kufundishwa na idadi kubwa ya makocha msimu huu na hadi sasa makocha wanne tofauti wamesimamia benchi lao la ufundi.
Timu hiyo iliandaliwa na Ortega Deniran ambaye aliondoka kabla Fountain Gate haijacheza mechi hata moja ya Ligi Kuu na nafasi yake ikachukuliwa na Denis Kitambi.
Baadaye Kitambi aliachana nayo, akarithiwa na Mohamed Isamial ‘Laizer’ ambaye mwezi huu ameondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Fred Felix ‘Minziro’.
Yanga, Mbeya City, KMC, Singida Black Stars na Coastal Union zinafuatia kwa kunolewa na idadi kubwa ya makocha msimu huu na kila moja imekuwa chini ya usimamizi wa makocha watatu tofauti.
Yanga ilianza na Romain Folz, kisha ikawa chini ya usimamizi wa muda wa Patrick Mabedi na sasa iko chini ya Pedro Goncalves wakati Coastal Union ilianza na Ally Ameir akafuatia Mohamed Muya na sasa Fikiri Elias.
Mbeya City ilinolewa na Malale Hamsini baadaye ikamchukua Mecky Maxime na sasa iko chini ya kaimu kocha Patrick Mwangata ambaye ni kocha wa makipa wa timu hiyo.
Kwa upande wa KMC, kocha waliyeanza naye ni Marcio Maximo kisha ikawa chini ya Mohamed Abdallah ‘Baresi’ na sasa iko chini ya kaimu kocha, Imani Mwalupetelo.
Singida Black Stars ilianza kuwa chini ya Miguel Gamondi ambaye baada ya kuanza kuinoa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, akarithiwa na David Ouma na kwa sasa kocha mkuu ni Muhibu Kanu.
TRA United, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons na Mashujaa FC kila moja imekuwa chini ya makocha wakuu wawili kwa nyakati tofauti msimu huu.
Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ibrahim Masoud, amesema sababu ya mabadiliko ya mara kwa mara kwa mabenchi ya ufundi ni vitu viwili ambavyo ni matarajio na mahitaji.
“Hii ni kazi ya taaluma ambayo inahitaji kila dakika kujifungia ndani kufanya tathmini. Sasa ukija kwa msimu huu, wanasema kama ukianza vibaya kwa maana ya maandalizi ya msimu basi utafeli tu.
“Kwa msimu huu mabadiliko ya walimu yamechangiwa kwanza na mahitaji ya timu. Timu kama Simba na Yanga zina mahitaji makubwa sana, hivyo kocha anayekuja anatakiwa afikie mahitaji ya viongozi.
“Pia mpira huu sasa umeingiliwa na mambo mengi. Mpira kama mpira katika nchi, matarajio na mahitaji ndio vitu ambavyo vimeingia kwa sana. Mwalimu anaweza asihukumiwe kwa kufungwa na Simba na Yanga lakini pale wanapokutana na timu za madaraja yao na kupoteza ndiyo shida inapokuja. Kwenye matokeo mabaya hakuna mwalimu anayeweza kuvumiliwa lakini wanachoshindwa ni kujifikiria kwamba hao wanaomuajiri mwalimu wanaweza kufikia matarajio?” amesema Masoud.
Kocha wa viungo wa KMC, Uhuru Selemani, amesema ukocha ni taaluma yenye presha na mahitaji makubwa.
“Kuna wakati wachezaji wanakuwa hawafanyi vizuri lakini mwisho wa siku kocha ndio unakuja kuwajibika, hivyo ni jambo la kawaida kutokea,” amesema Uhuru.
